Windows

Serikali yatoa Bilioni 2.5 ujenzi wa jengo la mama na mtoto


Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imetoa kiasi cha shilingi bilioni 2.5 zitakazotumika katika ujenzi wa jengo la mama na mtoto katika Hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, lengo likiwa ni kutoa huduma za kibingwa kwa akina mama wajawazito na watoto wachanga.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu wakati alipotembelea ujenzi wa Hospitali hiyo na kukuta jengo la wagonjwa wa nje (OPD) na Utawala likiwa limekamilika.

Waziri Ummy amesema fedha hizo zitafika katika Hospitali hiyo ndani ya wiki mbili ili ziweze kuchochea kasi ya ujenzi na lengo ifikapo mwezi Septemba 2019 Hospitali hiyo ianze kutoa huduma za afya.

“Ninaahidi kutoa shilingi bilioni 2.5 ndani ya wiki mbili ziweze kutumika katika ujenzi wa jengo la mama na mtoto, lengo la serikali ni kuhakikisha kila mama mjamzito anapofika Hospitalini kujifungua atoke akiwa salama yeye na kichanga chake”. Amesema Waziri Ummy.

Waziri Ummy amefikia uamuzi huo baada ya kupokea ripoti ya mkoa kuhusu vifo vitokanavyo na uzazi kutoka kwa Mganga Mkuu wa Mkoa Dkt. Mfaume Rashid, ambapo kwa mwaka 2016/2017 kulikua na vifo 73, na mwaka 2017/2018 vikiwa ni vifo 56, hali ambayo Waziri huyo ameonekana kutoridhishwa nayo.

Hata hivyo, Waziri Ummy ameahidi kuongeza fedha zingine kiasi cha shilingi bilioni 3 ndani ya mwezi mmoja, zitakazotumika katika ujenzi wa jengo kwa ajili ya huduma za uchunguzi ikiwemo huduma za maabara, X-ray na CT-Scan pia jengo hilo litakua na vyumba vitatu vya upasuaji.

Aidha, Waziri Ummy amehitimisha ziara yake katika mikoa ya kanda ya ziwa kwa kutembelea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga na kuridhishwa kwa kiasi kikubwa na hali ya utoaji wa huduma za afya hasa katika jengo la huduma za mama na mtoto na pia katika jengo la kuhifadhia watoto wachanga wenye uhitaji wa uangalizi maalumu (NICU)

Post a Comment

0 Comments