Windows

RC aagiza Shule ya Kata iliyoachwa kwa miaka 10 isajiliwe


Mkuu wa mkoa wa Rukwa Joachim Wangabo, amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi kuhakikisha Shule ya Sekondari ya Ntatepa iliyopo kata ya Myula, Wilayani Nkasi inasajiliwa mwezi wa tatu mwaka 2019 ili kuanza kuchukua wanafunzi wa kidato cha kwanza ambao watahamishwa kutoka shule za kata za jirani na hatimae kuwapunguzia umbali wa kutembea wanafunzi wanaotoka katika kata hiyo kwenda kata za jirani kusoma.

Mkuu huyo amesema kuwa ili kuhakikisha kasi ya ujenzi wa shule hiyo inaongezeka atachangia bati 100 na kuwataka viongozi wote wa Serikali za Vijiji vitano vinavyounda kata hiyo vyenye kaya 2547 kuhakikisha kila kaya inachangia shilingi 5000 ili kukamilisha ujenzi wa shule hiyo ambao ulianza mwaka 2008 na kuwekwa jiwe la msingi mwaka 2013 na aliyekuwa Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Aggrey Mwanri.

“Mimi inaniuma sana kuona tangu mwaka 2008 hii shule, haijaanza, haijasajiliwa, lile jengo pale la waalimu nimesoma pale lile jiwe la msingi liliwekwa na Mwanri wakati huo akiwa Naibu Waziri TAMISEMI mwaka 2013 leo hii ni mkuu wa Mkoa wa Tabora, najisikia vibaya, miaka mingi 11 shule haianzi, basi na ianze mwaka huu, nitumie nafasi hii kuwahamasisha wanakata wote wa Myula, tuchangie shule imlizike,” Alisema.

Aliyasema hayo Januari 11 mwaka huu alipotembelea shule hiyo ili kubaini mkwamo uliopelekea shule hiyo kushindwa kusajiliwa na kuweza kusomesha wanafunzi, Aidha Wangabo alirudi tena tarehe 22.1.2019 kufanya harambee ili kupata fedha za kufanya ukarabati wa madarasa manne ya wanafunzi, nyumba ya mwalimu mkuu ambayo ilikuwa tayari pamoja na kumalizia madara mawili na maabara ambayo ilikuwa ndio kikwazo cha kusajiliwa kwa shule hiyo.



Post a Comment

0 Comments