Windows

MESSI AIBUA MAPYA KARNE YA 21



Lionel Messi

MKALI wa soka duniani, Lionel Messi amezua mapya tena kwenye medani ya soka baada ya kuibuka na rekodi nyingine.



Messi alianzia kwenye benchi wakati timu yake ya Barcelona ilipovaana na Leganes kwenye mechi ya La Liga, wikiendi iliyopita.



Hata hivyo, licha ya kuingia kipindi cha pili kama `sub’(mchezaji wa akiba) bado alipiga bao wakati Barcelona ilipoichapa Leganes 3-1.



Bao hilo lilifanya Messi aweke rekodi nyingine ya La Liga kutokana na kuwa `sub’ aliyefunga mabao mengi zaidi kwenye karne ya 21.

Ni wazi kuwa Messi hata akianzia kwenye benchi bado ni moto likija suala la kufanya mambo makubwa kwenye soka.



Sio siri kuwa Messi ana rekodi kibao za soka, ambapo ni hivi karibuni alifikisha mabao 400 kwenye La Liga.

Wakati bado mashabiki wa soka wakitafakari rekodi yake ya mabao 400, Messi ameibuka na rekodi nyingine kama `sub’.



Sasa ni mchezaji, ambaye amefunga mabao mengi zaidi akiwa kama `sub’ kwenye mechi za La Liga katika karne hii ya 21.

Kocha wa Barcelona, Ernesto Valverde aliamua kumwanzisha nahodha wake Messi kwenye benchi katika mechi ya La Liga dhidi ya Leganes.



Messi aliingia baada ya kuwa Leganes ilikuwa imepata bao la kusawazisha kupitia kwa Martin Braithwaite.

Staa huyo wa Argentina aliisaidia Barcelona kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 kwa kupachika bao moja huku mengine yakipachikwa na Ousmane Dembele na Luis Suarez.



Messi alipiga bao la tatu la Barcelona kwa ufundi mkubwa kwenye dakika za majeruhi za mchezo huo.

Staa huyo mwenye umri wa miaka 31 aliweka rekodi ya kufunga mabao 25 msimu huu huku akifikisha bao la 401 la La Liga.



REKODI KAMA `SUB’

Pamoja na kuwa imezoeleka kwa Messi kuanza kwenye ‘first eleven’(kikosi cha kwanza) ya mechi za timu yake lakini pamoja na mara chache anazoanzia kwenye mechi kama `sub’ bado pia ameandika historia.

Bao lake la kwenye mechi dhidi ya Leganes limemfanya aweke rekodi kama `sub’.



Messi mwenye rekodi ya kunyakua tuzo ya mwanasoka duniani mara tano, amefunga mabao 22 kwenye La Liga akitokea kwenye benchi ambapo hakuna staa aliyefikisha mabao hayo kwenye karne ya 21.

Hiyo ni rekodi kwa La Liga na hata ligi nyingine Ulaya kwani hakuna staa aliyefikisha idadi hiyo kubwa ya mabao akiwa kama `sub’.



Hata hivyo, Messi ameifungia Barcelona jumla ya mabao 34 na kutoa asisti tano kwenye mechi 76 za mashindano mbalimbali ambazo Messi ameingia kama `sub’.

Baada ya kuweka rekodi hiyo, Messi anafukuzia rekodi ya Mfalme wa soka duniani, Pele ambayo imedumu tangu mwaka 1974.



Mbrazili alipachika mabao 619 wakati akichezea Santos ya Brazil wakati Messi amepachika mabao 588 katika mechi 660 za mashindano mbalimbali alizoichezea Barcelona.



Messi akiwa na umri wa miaka 31 tu, sasa ana uwezo wa kufukuzia rekodi ya staa wa zamani wa Czech, Josef Bican.

Bican katika kipindi akisakata soka kuanzia mwaka 1928 hadi 1955, alipachika jumla ya mabao 500 kwenye Ligi Kuu ya Jamhuri ya Czech.



Hata hivyo, kuna wakati alicheza kwenye Ligi Kuu Austria, ambako alifunga mabao kadhaa na kufanya awe na jumla ya mabao 603 ya ligi mbili yaani ukijumuisha na ile ya Czech.

Bican katika enzi zake akisakata soka alifunga jumla ya mabao 1468 kwa ligi na mashindano mbalimbali.

Post a Comment

0 Comments