Msimu mpya wa mashindano ya SportPesa unaendelea Jijini Dar es Salaam. Kesho unaingia kwenye hatua yanusu fainali. Ni mashindano yanayoshirikisha timu za Tanzania na Kenya ambazo zinachuana kwa kipindi kifupi sana.
Tanzania iliwakilishwa na Yanga, Simba, Singida na Mbao. Kabla ya mechi za Simba na Mbao jana, Yanga na Singida tayari walishaaga mashindano.
Ni Mashindano ya wiki moja lakini yenye umuhimu mkubwa kibiashara na kiuchumi kwa upande wa klabu zetu ambazo zinashiriki Ligi Kuu Bara isiyo na mdhamini mkuu mpaka sasa.
Bingwa wa michuano hiyo mbali na kupata nafasi ya kucheza na Everton ya England na kwenda Ulaya kula bata na kucheza na Everton bado anapata fedha nyingi.
Mshindi anapata Mil 70 ambazo kwa klabu inayojiendesha kibiasahara ni fedha nyingi ndani ya siku 7 tu. Ndio maana klabu na wachezaji wa Kenya mara zote wamekuwa wakipiga hesabu kali sana kwenye mashindano hayo huku Watanzania tukibaki kuyachukulia ya kawaida.
Maoni yetu ni kwamba klabu zetu ziamke,ziwe zinakazania fedha hizo kutokana na hali halisi iliyopo kwenye soka la Tanzania kwasasa.
Ligi yetu ina matatizo mengi ambayo yanatokana na kutokuwa na mdhamini ambapo mpaka sasa hakuna uhakika wa zawadi mwisho wa msimu.
Hivyo basi ni jambo la busara sana kama wawakilishi wa Tanzania wangetumia wiki moja kutengeneza fedha hizo ambazo ni nyingi tena kwa muda mfupi. Lakini matokeo yake wengi wamechemsha.
Walipaswa kuyatazama mashindano hayo kwa jicho la kibiashara zaidi na kupata mzuka wa kupambana, jambo ambalo lingesaidia kuitangaza zaidi ligi yetu kwavile wapo mawakala wa sehemu mbalimbali.
Uwepo wa klabu kama Gor Mahia,AFC Leopards, Kariobangi na Bandari tulitegemea iwe changamoto kubwa kwa timu zetu za Tanzania katika kujipima uwezo na kujiimarisha tayari kwa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara.
Timu za Kenya hazina utani kwenye mashindano kama hayo ambayo mashabiki wengi wanayachukulia kama bonanza. Timu zetu zijifunze kuheshimu mashindano yoyote yenye fedha na ushindani mkubwa kama haya ya SportPesa. Mara zote tumekuwa tukiyapuuza na kushuhudia Wakenya wakicheza fainali na kuendelea kugawana utajiri na zawadi mbalimbali na ndio kinachokwenda kutokea sasa.
Kufanya vizuri kwa klabu za Tanzania,kungeweza kushawishi hata SportPesa wakaamua kujiingiza kwenye udhamini wa Ligi Kuu Bara kwavile sehemu hii ndiyo yenye ushabiki mkubwa wa soka kwa sasa.
Hakuna mfanyabiashara ambaye hapendi kujihusisha na kitu kizuri ili ajitangaze.
Hivyo tunazisihi klabu zetu kuongeza mapambano na ushindani katika sehemu mbalimbali zinapoalikwa kushiriki michuano kama hii ya SportPesa wasiishie kucheza kama mechi za kirafiki.
Kilichozikuta timu zetu zilizoondolewa mapema kwenye michuano hiyo ni tabia ya wachezaji wetu kudharau na kuchukulia mambo kirahisi bila kujua kila sekunde kwenye mchezo ni kitu muhimu.
0 Comments