Windows

HOFU: Neymar hatarini kuikosa Man United Ulaya



INAWEZA kuwa moja kati ya habari njema ambazo mashabiki wa Manchester United na benchi lao la ufundi wamepokea mwaka huu. Mechi ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya PSG hatua ya mtoano imekaribia na kuna uwezekano kwamba Wafaransa hao wakashuka uwanjani bila ya staa wao, Neymar.


PSG imethibitisha Neymar ameumia mfupa laini wa juu ya kifundo cha goti ambao nusura umkoseshe michuano ya kombe la dunia na kuna uwezekano akakosa mechi hiyo muhimu huku mashabiki wa United wakishangilia kimya kimya.


Juzi jumatano staa huyo nahodha wa Brazil alitolewa uwanjani akichechemea baada ya saa moja wakati PSG ikishinda pambano lao la kombe la Ligi dhidi ya Strasbourg na kocha wa PSG, Thomas Tuchel alikasirika akidai kwamba mwamuzi hakumlinda Neymar katika mechi hiyo.


Hata hivyo majeraha ya Neymar yalikuja bila ya staa huyo kuguswa na mchezaji yeyote wa timu pinzani lakini kocha wa Strasbourg, Thierry Laurey pamoja na wachezaji wake walimlaumu Neymar kwa kucheza kwa mbwembwe nyingi uwanjani bila ya kuonyesha heshima kwa wapinzani wake na wamedai staili yake hiyo inaalika rafu kutoka kwa wapinzani.


Ingawa hakuumia kutokana na rafu za wapinzani wake lakini Neymar alichezewa rafu nyingi katika pambano hilo na kiungo wa Strasbourg, Anthony Goncalves, ambaye naye alimchubua Neymar katika pambano hilo hakuonyesha huruma yoyote kwa staa huyo kuumia huku akidai kuwa ilikuwa ni malipo kwa tabia yake ya kijinga uwanjani.


“Ni staili yake, lakini kama ukicheza kwa namna hiyo usimlaumu yeyote kama ukiwa unagongwa uwanjani. Ni mchezaji mkubwa na namuheshimu kwa jinsi alivyo lakini hatupo hapa ili yeye ajifurahishe. Hatuko hapa kumfanya yeye aonekane bora.” Alisema Goncalves.


Na sasa Tuchel pamoja na PSG wanasubiri kwa hamu kujua Neymar ameumia kwa kiasi gani. taarifa ya PSG mapema jana Alhamisi ilisema matibabu ya Neymar yatategemea na namna gani mguu wake utakavyokuwa unaendelea katika siku chache zijazo.


PSG inasafiri kwenda kucheza na Manchester United katika pambano la kwanza Februari 12 na tayari wanahaha kujua hali ya kiungo wao wa kimataifa wa Italia, Marco Verratti ambaye aliumia kifundo cha mguu wikiendi iliyopita.


“Neymar ana wasiwasi kwa sababu ni mguu ule ule na eneo lile lile aliloumia kabla ya kombe la dunia. Kwa sasa hakuna habari zaidi, amekwenda hospitali. Nahitaji kuongea na Daktari anipe habari zake. Mwamuzi hakupiga filimbi alipochezewa madhambi mara moja, mbili, halafu mara tatu, mpaka alipojiumiza mwenyewe.” Alisema Tuchel.


Marudio ya picha za televisheni yanamuonyesha Neymar akikunja mguu wake kwa bahati mbaya ardhini ikiwa ni mwaka mmoja tangu aumie kwa staili hiyo katika pambano la ligi dhidi ya Marseille na nusura akose kombe la dunia. Aliondoka uwanjani akiwa Analia.


Naye kocha wa Strasbourg, Laurey aliungana na wachezaji wake akisema “Anajiharibu mwenyewe, hiyo ni staili yake na nadhani watu wanakuja kutazama hilo. Lakini asije kulalamika baadae kama ambavyo amekuwa akifanya. Ni sehemu ya silaha yake na sisi tuna silaha zetu.”


“Wakati mwingine unapozidisha inabidi upambane na hali yako. Huwa nawaelewa wachezaji wangu wanaposhindwa kuvumilia wachezaji ambao wanawanyanyasa uwanjani. Baada ya muda lazima uwaonyeshe. Siku zote napenda kuwalinda wachezaji lakini kuna mipaka yake.” aliongeza kocha huyo.


Mlinzi mwingine wa Strasbourg, Pablo Martinez aliongeza kwa kusema “Ni kweli ni mchezaji mahiri sana, lakini kutokana na tabia zake ni mchezaji ambaye simpendi uwanjani. Licha ya kujaribu kukunyanyasa lakini pia huwa anaongea vibaya.”


Post a Comment

0 Comments