WAKATI michuano ya Sport Pesa leo Ijumaa ikiendelea hatua ya nusu fainali ambapo Simba itacheza na Bandari ya Kenya huku Mbao FC wataumana na Kariobangi Sharks, makocha Mwinyi Zahera wa Yanga na wa Simba, Patrick Aussems wameshapishana mlangoni pale Uwanja wa Taifa.
Lakini kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera alisema ili Tanzania ioneshe kuwa na uwezo wa soka katika mashindano ya SportPesa lazima timu kutoka nchini ibebe ubingwa huo ambao mara mbili mfululizo ulienda Kenya ukichukuliwa na Gor Mahia waliovuliwa ubingwa huo na Mbao FC juzi.
Zahera alisema katika mashindano hayo zimebakia timu mbili za Tanzania ambazo anaziombea kila lenye kheri ili zifanye vizuri na kati ya hizo moja itwae ubingwa.
“Naitakia kila la kheri Simba na wala sina tofauti nayo yoyote kwa timu yao ilivyo nzuri naamini wanaweza kushindana na wakatwaa ubingwa ambao utakuwa faida kwa ligi yetu.
“Unajua wakati mwingine si jambo jema mara zote ubingwa unakwenda Kenya,” alisema Zahera.
Wakati Zahera akiitakia mafanikio Simba huku yeye akiwa ametolewa kwenye mashindano hayo kocha wa Simba, Patrick Aussems alisema anatumia mashindano hayo kama maandalizi ya mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly itakayochezwa Februari Mosi.
“SportPesa ni wadhamini tunawaheshimu na tunatambua fika tukifanikiwa kuwa mabingwa wa mashindano haya miongoni mwa zawadi ambazo tutapata ni wachezaji wangu kucheza na timu kubwa ya Everton ya Uingereza,” alisema Aussems.
0 Comments