Windows

Kesi uchaguzi Yanga: Bodi ya wadhamani yaitwa Mahakamani

 Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeamuru Bodi ya Wadhamini wa klabu ya Yanga, itangazwe gazetini kama njia ya wito wa kufika mahakamani hapo kwa ajili ya kesi ya kupinga uchaguzi ndani ya klabu hiyo iliyofunguliwa na wanachama wawili.
Amri hiyo ilitolewa leo na Hakimu Mkazi Mkuu, Janeth Mtega, kufuatia maombi yaliyotolewa na wakili wa walalamikaji, Daud Mzeri, akidai kuwa imekuwa vigumu kwa mdaiwa huyo kupoikea hati ya wito iliyotolewa na mahakama.
Kesi hiyo ya kikatiba namba 1 ya mwaka 2019, imefunguliwa na wanachama wawili wa Klabu ya Yanga, Juma Magoma na Athuman Nyumba, wanapinga kufanyika kwa uchaguzi huo kwa madai kuwa unakwenda kinyume na katiba ya klabu hiyo.
Kesi hiyo iliyofunguliwa Januari 11, mwaka huu ilitajwa kwa mara ya kwanza mahakamani hapo leo, lakini wadaiwa wote wawili hawakuwepo mahakamani.
Mbali na Bodi ya Wadhamini wa Klabu ya Yanga, mdaiwa mwingine katika kesi hiyo ni Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka nchini (TFF), mdaiwa wa kwanza.
Wakati kesi hiyo ilipotajwa, Wakili Mzeri aliieleza mahakama kwamba wadaiwa wote leo hawajafika mahakamani na mdaiwa wa pili (Bodi ya Yanga) amegoma kupokea wito.
“Hivyo tunaomba reservice (kupeleka tena hati ya wito) kwa ajili ya second respondent (mdaiwa wa pili). Pia tuna ku- substitute kwa publication (kuchapisha gazetini) kwa sababu imekuwa vigumu kwa huyu second respondent kupokea summons (hati ya wito) yetu,” alisema Wakili Mzeri.
Hakimu Mtega alikubaliana na maombi hayo na akaamuru mdaiwa wa pili (Bodi ya Yanga) atangazwe gazetini kama njia ya wito wa kufika mahakamani na pia akaamuru mdaiwa wa kwanza (TFF) awasilishe utetezi wake.
Hakimu Mtega aliahirisha kesi hiyo hadi Februari 11, mwaka huu, kesi hiyo itakapotajwa tena mahakamani hapo.
Uchaguzi huo ulipangwa kufanyika Januari 13, 2019, kwa lengo la kujaza nafasi mbalimbali zilizoachwa wazi, lakini ulishindikana kutokana na kufunguliwa kwa kesi hiyo.
Katika madai yao Magoma na Nyumba wanapinga kufanyika kwa uchaguzi huo kwa madai kuwa unakwenda kinyume na katiba ya Klabu ya Yanga ya mwaka 2010 ibara ya 7.
Ibara hiyo inaelezea utaratibu wa uanachama ndani ya Klabu ya Yanga ambao, kwanza ni kutuma maombi, ambapo maombi hayo yatapelekwa kwa Katibu Mkuu wa Klabu ya Yanga, ambaye baaade yatajadiliwa na kamati tendaji.
Pia, ibara hiyo, inaelezea kuwa maombi hayo yataambatana na fomu namba YASC/U, ada ya uanachama ambayo ni Sh 12,000 pamoja ana ada ya kadi ambayo ni Sh 2000.
Pia wanadai kuwa kuna taarifa za kuwepo kwa wanachama wenye kadi feki za kieletroniki ambazo zina saini na mhuri ambazo zinasambaa kwa baadhi ya wanachama, ambazo zinaonyesha kuwa zimetolewa na benki ya CRDB pamoja na benki ya Posta.
Wanadai kuwa kadi hizo zinazodaiwa kuwa ni kadi za uanachama wa Klabu ya Yanga, zikiwa na picha za wamiliki ambazo sio mali ya klabu hiyo.
Hivyo wanapinga matumizi ya kadi hizo katika uchaguzi huo wakidai kuwa kwa namna yoyote ile haziwezi kuwa uthibitisho wa uanachama wa Yanga, kwa kuzingatia kwamba, wahusika wa hizo kadi, hawakupitia utaratibu ulioanishwa katika ibara ya 7 ya mwaka 2010 ya klabu ya Yanga.

Post a Comment

0 Comments