Windows

Duh! Bellerin ndo basi tena

ARSENAL ya Ligi Kuu England imepata pigo baada ya beki wake pembeni, Hector Bellerin kupata majeraha mabaya ya goti ambayo yatamfanya kukosa msimu wote 2018/2019.
Bellerin alipata na majeraha haya kipindi cha pili katika mechi ngumu iliyochezwa Jumamosi na dhidi ya Chelsea na timu yake kuibuka na ushindi wa mabao 2-0.
Taarifa za kitabibu zinaonyesha mchezaji huyu amepata jeraha la goti la kushoto kwa kukwanyuka nyuzi ngumu ya ligamenti iliyopo mbele ya goti.
Kitabibu nyuzi hii inajulikana kama Anterior Cruciate Ligament (ACL) ndiyo mhimili wa ungio la goti ikiwa eneo la katikati ikiunganisha mfupa mkubwa wa paja na wa chini ya goti.
Jeraha alilolipata la ligamenti linaainishwa kama daraja la tatu ambapo nyuzi hiyo hukatika pande mbili na kuachana au kukwanyuka katika mfupa uliojipachika.
Kwa kawaida majeraha ya ligamenti huanishwa katika aina tatu, aina ya kwanza huwa ni kujivuta kupita kiwango na kuchanika pasipo kuachana pande mbili.
Daraja la tatu huwa ni jeraha baya linalohitaji upasuaji kama sehemu ya matibabu jambo linalochangia mchezaji kukaa nje ya uwanja kwa muda mrefu akiuguza jeraha la upasuaji.
Jeraha hili huwa ni kubwa na huambatana na maumivu makali hali iliyomfanya Bellerin kulia kwa maumivu huku akilishikilia goti hilo. Aina hii ya majeraha huweza kuchukua muda mrefu kupona na kurudi tena uwanjani. Jeraha hili linaweza kumweka nje kwa zaidi ya miezi tisa hadi mwaka mzima.
Aina hii ya jeraha ndilo lililompata mchezaji wa Liverpool, Alex Chamberlain ambaye tangu Aprili mwaka jana ndio sasa anatazamiwa kurudi uwanjani.
Hivyo, ni dhahiri Mhispania huyo hataonekana tena katika msimu na kuacha pigo lingine katika ukuta wa Arsenal ambao una majeruhi wengi. Bellarin ameishafanyiwa vipimo muhimu ikiwamo picha ya MRI ambayo inatoa taswira nzuri juu ya vitu vilivyomo katika ungio la goti na kubaini kwa kina ukubwa wa jeraha.
Wakati wowote anaweza kuingia chumba cha upasuaji kwa lengo la kuzikarabati nyuzi na kuirudishia mahala pake.  Katika mechi aliyoumia alitoa mchango mkubwa katika ushindi huo ikiwamo pasi aliyotoa kwa Alexandre Lacazette ndiyo ilizaa bao la kwanza dakika ya 14.

Bellarin alivyoumia Majeraha ya goti ni vigumu kuyaepuka hasa kwa wachezaji wa soka.  Taarifa sahihi zinasema wanasoka ndio wanaongoza kupata majeraha ya aina hii wakifuatiwa na wachezaji wa mpira wa kikapu na rugby.
Kama vile haitoshi majeraha ya goti yanashika nafasi ya tatu kati ya majeraha yanayowakumba wachezaji wa Ligi Kuu England.
Katika mechi ile iliyokuwa na ushindani mkali Bellerin alikuwa akipanda kushambulia na kurudi kwa kasi kukaba, hata jeraha lilimpata akiwa eneo la kati akijaribu kuwania mpira ili ashambulie.
Mguu wa kushoto ulitua vibaya na kujipinda uelekeo, hivyo ungio la goti lilipata shinikizo kubwa kutokana na utuaji ambao sio mjengeo wa kawaida wa goti.
Mara nyingi ligamenti hii inapata majeraha mara baada ya mtu kuchomoka kwa kasi na kujipinda ghafla au kutua ghafla goti likiwa limenyooka au kujipinda kidogo kama ilivyotokea kwa Bellarin.
Ishara kubwa inayoaishiria nyuzi ya ACL imejeruhiwa ni kusikia mlio fulani ndani ya goti unaojulikana kitabibu kama Popping Sound.
Takwimu za majeraha ya michezo zinaonyesha karibu 70% ya mejaraha ya nyuzi za ACL huwa si kwa kufanyiwa faulu wala kugongana na mpinzani, bali mchezaji mwenyewe kujijeruhi kwa kujipinda vibaya.
Nyuzi ngumu za ACL ziko kama herufi ‘x’ kazi yake ni kuzuia mifupa inayounda ungio la goti kutulia katika eneo lake na isiteleza kwenda upande wa nyuma na vilevile kuliwezesha goti kujizungusha.
Ikumbukwe goti lina mijongea mikuu mitatu ikiwamo kunyooka, kupinda kutoka mbele kuja nyuma na kujizungusha.  Hivyo basi, uelekeo mwingine wowote nje ya hii huweza kusababisha majeraha.
Bellerin alifanyiwa huduma ya kwanza uwanjani baada kuwepo viashiria ya kuumia huku wachezaji wa pande zote mbili wakihimiza  apewe huduma ya kwanza.
Alihudumiwa uwanjani kwa dakika kadhaa kisha akatolewa nje akiwa amebebwa kwa tahadhari ya hali ya juu kwa lengo la kulinda mguu usijijeruhi zaidi.
Aliwekwa katika machela maalumu na mguu uliojeruhiwa akilindwa kwa kuweka kifaa tiba kinachokaba na kutuliza mguu usitikisike. Nafasi yake ilichukuliwa na Ainsley Maitland-Niles.
Tukio hili la uwanjani na mtiririko wote mpaka Kocha Unai Emrey kupewa ishara kuwa afanye mabadiliko lilikuwa ni ishara ya mapema kuwa Bellerin amepata jeraha baya hata ya kuchunguzwa kwa vipimo.
Baada ya kubainika amepata jeraha hilo mchezaji huyo ameweka wazi kuwa yuko tayari kukabiliana na changamoto yoyote itakayokuja mbele yake.
Ingawa nafasi yake inaweza kuzibwa na Ainsley Maitland-Niles au Nacho Monreal lakini tayari Kocha Emery ameiomba klabu yake kusajili beki atakayeziba pengo lake.
Beki huyo Mhispania  mwenye umri wa miaka 23 atanyiwa upasuaji siku chache zijazo.
 Wachezaji na mashabiki wametumia muda mwingi kumfariji akiwamo na nahodha wa Arsenal aliyerudi kutoka katika majeraha, Laurent Koscielny.

Post a Comment

0 Comments