Windows

Yaliyoibeba Yanga SC kwa Alliance FC, msoto bado mkali

Mwanaspoti-Yaliyoibeba-Yanga SC-Alliance FC-Tanzania-msoto-bado-mkali Yanga juzi iliendelea kudhihirisha kuwa bora mbele ya Alliance kufuatia ushindi wake wa nne mfululizo tangu wakutane tangu msimu uliopita kwenye michezo minne ikiwamo ya Kombe la Shirikisho.

Mabingwa hao wa zamani wa Ligi Kuu Bara wakicheza katika ubora wao chini ya kaimu kocha mkuu, Boniface Mkwasa waliendeleza furaha kwa mashabiki wao kutokana na matokeo mazuri waliyoyapata ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya wenyeji wao.

Kama haitoshi ushindi huo ulikuwa wa tatu mfululizo kwa Mkwasa aliyepewa majukumu baada ya aliyekuwa kocha mkuu wa timu hiyo Mwinyi Zahera kufungashiwa virago.
Mbali na ushindi huo wa Yanga mtamu, lakini haukuwa rahisi kivile kutokana na ushindani walioupata na kama wasingetumia uzoefu na juhudi binafsi za wachezaji mmoja mmoja, huenda nyota nje isingeangukia upande wao.

Mwanaspoti ambalo lilikuwa makini kufuatilia mpambano huo uliopigwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza linakuletea sababu zilizoipamba Yanga kushinda mechi hiyo, udhaifu ulioonekana pamoja na upande wa Alliance.

Nje ya uwanja
Matokeo ya ushindi wa Yanga yalianzia nje ya uwanja kutokana na mashabiki walichokuwa wakifanya tangu timu hiyo ilipotua jijini hapa kwa ajili ya mchezo huo.
Yanga ilipotua Mwanza Jumatano asubuhi, ilienda moja kwa moja kupumzika katika Hoteli ya Jawita iliyopo katikati ya jiji, lakini jioni ilipiga tizi la ‘kufa mtu’ kwa saa tatu hadi giza lilipoingia.
Mbinu walizotumia zilikuwa wazi Alliance kuumia kwani mashabiki wa Yanga waliamua kuipeleka timu hiyo kufanya mazoezi kwenye Uwanja wa Chuo cha Ualimu Butimba na ukikumbuka uwanja huo umekuwa na bahati kwa vigogo hao wa soka hapa nchini.

Ikumbukwe kuwa kipindi walipokuja Mwanza kuweka kambi kwa ajili ya mchezo dhidi ya Mbao FC kusaka ushindi wa kwanza na pia dhidi ya Pyramids ya Misri kwa ajili ya kufuzu Ligi ya Mabingwa Afrika, walikuwa wakifanyia mazoezi uwanjani hapo chini ya Zahera na kufanikiwa kuvunja uteja kwa Mbao FC licha ya kwamba Pyramids iliwadondoshea kichapo cha mabao 2-1. Kama haitoshi,Yanga walitumia akili nyingi kusaka baraka za wagonjwa walipokwenda kutoa misaada katika Hospitali ya Rufani Bugando saa chache kabla ya kushuka uwanjani.

Pia, nguvu ya mashabiki kwa Alliance ilikuwa ndogo ukilinganisha na Yanga ambao muda wote walikuwa pamoja wakipanga mbinu za kumaliza mechi hiyo mapema.
Kadhalika, uwapo wa hamasa ya Sh10 milioni uliwachagiza zaidi wachezaji wa Yanga kupambana kwa dakika 90 ili kuhakikisha wanashinda. Pesa hizo zinatolewa na mmoja wa wadhamini wao kampuni ya GSM. Hiyo ilikuwa nje ya uwanja na pia ndani kwa kiasi fulani.

Ndani ya uwanja
Katika mchezo huo licha ya ushindani mkali kwa timu zote, lakini kipindi cha kwanza Yanga walionekana kumiliki kabumbu kwa asilimia kubwa kuliko wapinzani wao.

Tatizo la Alliance FC kujaa presha mapema liliwapa mwanya Yanga kulazimisha mashambulizi ambayo yaliwapa faida kwa kujipatia bao dakika ya 25 lililofungwa na Patrick Sibomana.
Alliance FC walijaribu kurudi kipindi cha pili kwa kushambulia zaidi, ambapo licha ya Yanga kuonekana kutakata eneo la katikati, lakini sehemu ya beki ilipwaya hasa beki wake, Lamine Moro ambaye pasi zake zilikuwa haziendi mbali.

Hatua hiyo iliwapa nafasi Alliance FC kupeleka mashambulizi mfululizo langoni mwa Yanga na kufanikiwa kusawazisha katika dakika ya 54 kupitia kwa Juma Nyangi.
Kuingia kwa bao hilo kulionekana kuwaamsha zaidi wababe hao wa Jangwani ambao walilazimika kubadili mbinu kwa kumtoa beki wa kushoto Jafari Mohamed na kumuingiza Mrisho Ngasa ili kuongeza mashambulizi.

Mbinu hizo za Mkwasa zilizaa matunda kwani katika dakika ya 71 walijiongezea bao la pili lililowekwa wavuni na David Molinga aliyefikisha mabao matano msimu huu.

Straika Yanga bado
Pamoja na ushindi huo, lakini Yanga itapaswa kujitathmini hasa kuelekea kwenye dirisha dogo la usajili kuhakikisha inatazama safu yake ya ushambuliaji ikiwezekana kuiongezea nguvu.
Katika mchezo wa juzi dhidi ya Alliance FC, timu hiyo ilitengeneza mashambulizi mengi na nafasi kadhaa za kufunga, lakini ubutu wa mastraika ulionekana kuitesa kutokana na kushindwa kumalizia vyema mipira ya mwisho.

Yanga kama ingekuwa na safu kali ya ushambuliaji ingeweza kuibuka na ushindi wa zaidi ya mabao mawili iliyopata kutokana na nafasi nyingi walizopata kina Molinga na Sadney Urikhob kushindwa kuzitumia.

Pia, tatizo la Yanga lilikuwa kwenye sehemu ya beki kwani ilishuhudiwa kuruhusu wavu wao hasa kipindi cha pili licha ya kutangulia kupata bao na kujikuta wakifungwa.
Ukiachana na mechi ya juzi dhidi ya Alliance FC, hata mchezo wao na JKT Tanzania walitangulia kufunga mabao 3-1 hadi mapumziko, lakini hadi dakika 90 ubao wa matangazo uwanjani ulisomeka 3-2.
Hivyo kutokana na upungufu hao, iwapo benchi la ufundi halitashtuka kufanya mabadiliko kwa kipindi cha dirisha dogo, huenda ile dhana ya kutumia uzoefu kupata matokeo ikawatesa huko mbeleni.

Kwa upande wa Alliance FC walistahili pongezi kutokana na uchanga wao kwenye Ligi Kuu na kufanikiwa kuwabana Yanga huku wakifuta kidogo machungu ya matokeo waliyopata kwa Azam FC iliyowalaza mabao 5-0.

Makocha watoa ya mioyoni
Kaimu kocha mkuu wa Yanga, Charles Mkwasa alikiri kuwa licha ya kufanikiwa kupata ushindi, lakini mambo hayakuwa rahisi kutokana na ‘mziki’ waliokutana nao kutoka kwa Alliance FC.
Alisema kama wasingekomaa kwa wapinzani wao mambo yangekuwa tofauti, lakini umakini na utulivu wa nyota wake ulisaidia kufikia malengo yao.

“Tulikuja kwa tahadhari kwa sababu Alliance walikuwa wamepoteza mechi iliyopita (dhidi ya Azam FC), kwa hiyo nikawaambia wachezaji nini wafanye nao wakatekeleza, ila tumepata ushindani mkali,” alisema Mkwasa.
Kwa upande wake, kocha wa Alliance FC, Kessy Mzirai alisema walipambana vilivyo dhidi ya Yanga, ila mambo yalikuwa magumu na kwamba makosa yaliyojitokeza watayafanyia kazi.
“Vijana wangu walionyesha ushindani, lakini walishindwa kupata matokeo mazuri, tumecheza na timu kubwa, makosa yameonekana na sisi benchi la ufundi tutayafanyia kazi,” alisema kocha huyo.

Post a Comment

0 Comments