Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya klabu ya Simba Mohammed Dewji 'Mo' ambaye ni mwekezaji wa timu hiyo, amesema watafungua Simba Academy ambayo itakuwa na jukumu la kulea wachezaji wenye vipaji kwa ajili ya manufaa ya Simba
Akizungumza kwenye Mkutano wa Mwaka wa Wanachama wa Simba, Mo amesema vijana hao watafundishwa na kuwa wazalendo wa kweli wa klabu ya Simba
"Tuna mpango wa kufungua Simba academy ili hapo badae tuje kuvuna vijana waliolelewa kwenye asili ya Simba
"Tuwafundishe vijana hao thamani ya Simba na falsafa ya uchezaji wa Simba, na sambamba upendo ili wawe na uchungu zaidi na klabu yetu," amesema Mo
Katika hatua nyingine, Mo amewatahadharisha wachezaji ambao wameonyesha nidhamu isiyoridhisha
Mo amesema umefika wakati wachezaji wanapaswa kufahamu ukubwa wa timu wanayocheza, hakuna nafasi ya kufanya mzaha
"Siridhishwi hata tone na nidhamu ya baadhi ya wachezaji wetu nje ya uwanja. Nimekuwa mnyonge kuona uwekezaji tuliouweka kwao, baadhi yao, huutumia kama fimbo ya kutuchapia"
"Niwaambie wachezaji wote, Simba ni klabu kubwa kweli kweli, tena kubwa hasa, na hakuna shaka ni namba moja Afrika Mashariki, bodi ninayoiongoza mimi haitavumilia mchezaji yoyote asiyejua thamani ya Simba. Kuonyana onyana sasa imetosha"
"Sisi tunawalipa vizuri mno, na wao wana wajibu wa kutulipa matokeo na furaha. Na ili furaha iwepo, lazima nidhamu isimamiwe kikamilifu, na katika hili hatutanii. Hatutajali ukubwa wa jina la mchezaji yoyote"
"Nidhamu kwetu ni muhimu kama tunataka tufikie malengo tuliyokusudia. Na haya ndio yaliyotufanya bodi tuchukue maamuzi magumu kwa kocha wetu. Timu imeshindwa kufikia malengo, kisha nidhamu hakuna, alafu tuvumilie?"
"Simba lazima tuamue kuteseka na moja katika mambo haya mawili, (1) tuzoee uchungu na maumivu ya nidhamu au (2) maumivu ya matokeo mabaya. Kama mpenzi wa Simba, siwezi"
"Mtaniwia radhi kidogo nimekuwa mkali ila nidhamu kwangu ndio kila kitu. Hata mimi mwenyewe naishi kwa nidhamu, na ndio siri ya mafanikio yangu, na naamini watu wote waliofanikiwa, na taasisi zote zilizofanikiwa msingi wake mkuu ni nidhamu ya kazi," amesema Mo
Kwa habari zaidi Download App ya soka kiganjani kutoka Play Store.
0 Comments