Windows

SIMBA MAMBO MOTO




KITENDO cha Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Senzo Mazingiza kuvamia mazoezi ya timu hiyo juzi, kimebadili hali ya hewa ndani ya kikosi hicho na kwamba kwa sasa mambo ni moto.

Mazingiza alitua katika mazoezi ya timu hizo juzi kwenye Uwanja wa Gymkhana, Dar es Salaam ikielezwa hakuwa ametoa taarifa hali iliyowashutia wachezaji na viongozi waliokuwapo uwanjani hapo.

Baada ya kufika mazoezini, Mzingiza alifanya mazungumzo na Meneja wa timu hiyo, Patrick Rweyemamu, ikiwamo kutaka kufahamu wachezaji waliokosekana na iwapo wameomba ruhusa.

Wakati anawasili uwanjani hapo, bosi huyo aliwakuta wachezaji watatu, Jonas Mkude, Clatous Chama na Pascal Wawa wakiwa nje ya uwanja ‘wakijikusanya’, wakati wenzao wakiendelea na mazoezi.

Baada ya wachezaji hao kumwona Mazingiza, waliingia uwanjani fasta na kuungana na wenzao kupiga tizi chini ya kocha wa muda, Dennis Kitambi.

Kitendo cha Mazingiza kufika mazoezini juzi, kimeonekana kuwashtua wachezaji na benchji la ufundi la timu hiyo na kwamba jana hakuna aliyeleta masikhara mazoezini kwani mara baada ya kufika uwanjani hapo, waliingia dimbani fasta na kuanza kujifua.

Kwa upande wao, Kitambi na wenzake wanaounda benchi la ufundi, walikuwa makini kusimamia mazoezi hayo, wakionekana kuhofia kukutwa na bosi wao huyo wakiwa ‘wanambwilambwila’.

Katika mazoezi ya jana yaliyoanza saa nne asubuhi, wachezaji walianza kwa kupigiana pasi fupi fupi na baada ya hapo kocha wao Kitambi, alipanga vikundi viwili na kuanza kuwafanyisha zoezi la kupiga pasi ndefu.

Wachezaji walifanya zoezi hilo kwa muda mrefu na kila walipokosea, Kitambi alikuwa akiwaambia warudie hadi pale walipoonekana wamepatia ikiwa pamoja na kukaba.

Zoezi hilo lilipomalizika walicheza mechi kufuatia walivyofundishwa kupiga pasi ndefu na kukaba pale adui alipofika eneo hatari.

Mara baada ya kumalizika kwa mazoezi hayo, Kitambi alisema anaendelea na programu ya mazoezi kama kawaida hadi hapo mwisho wa wiki hii, kama ambavyo uongozi ulivyompa majukumu.

“Tunaendelea na mazoezi kama kawaida siwezi kusema kuwa taendelea na mfumo wa siku zote kwa sababu hakuna timu ambayo tutaenda kukutana nayo ukizingatia tupo mapumziko,” alisema.

Alisema anaangalia zaidi sehemu ya mabeki ambako aliona mapungufu katika mechi mbili za mwisho walizocheza ikiwa dhidi ya Tanzania Prisons waliotoka suluhu pamoja na Ruvu Shooting ambao walipata ushindi wa mabao 3-0.

Post a Comment

0 Comments