Simba wiki ijayo huenda wakaingia katika historia nyingine kwa kuzindua rasmi matumizi ya viwanja vyao vya mazoezi vilivyopo Bunju nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Hii inakuwa historia kwa sababu klabu hiyo tangu izaliwe haikuwahi kufanya mazoezi katika uwanja wake ambao imeutengeneza yenyewe ukiacha kutumia kile kiwanja chao cha urithi pale Jangwani ambavyo hata hivyo ni kama vishapotea.
Kazi iliyofanyika pale Bunju ni hatua ya kila mdau wa klabu hiyo kujivunia kwani ndio dalili ya kuanza kuishi kisasa kwa klabu hiyo kama ambavyo mahitaji muhimu katika kuendesha timu ya soka yanavyoelekeza kwamba lazima kila klabu iwe na uwanja wakea angalau hata wa mazoezi.
Hali ilivyo inaonyesha Simba itakuwa na viwanja viwili kile cha nyasi za kawaida na kile cha nyasi bandia ambapo timu zao sasa za umri wote watakuwa na uchaguzi tu watumie kiwanja gani kulingana na kiwanja kipi wanakwenda kukitumia katika majukumu ya mechi zao.
Inawezekana wengi tukawa na nguvu ya kuupongeza sana uongozi wa sasa wa Simba juu ya mabadiliko ambao kimsingi ndio waliofanikisha umaliziwaji wa viwanja hivyo.
Ndiyo uongozi wa bodi ya Simba chini ya mwenyekiti wao Mohamed Dewji ‘MO’ ndio wanatakiwa kupongezwa kwa kusimamia kwa uthabiti ukamilifu wa viwanja hivyo mpaka sasa vikikaribia kuanza kutumika wiki chache zijazo.
Hata hivyo, bado kuna umuhimu mkubwa wa kutambua nguvu iliyofanywa na uongozi uliopita wa klabu hiyo katika kukamilisha ujenzi wa viwanja hivyo mpaka sasa.
Ikumbukwe Simba katika hatua hiyo walianzia mbali kwa kulipia eneo hilo kazi hiyo ilifanyika katioka uongozi wa Ismail Aden Rage ambaye licha ya kuwa na changamoto yake inawezekana hatua ya kulipia kodi ya ardhi ya eneo hilo ndio ambayo ilichagiza mafanikio hayo na sasa eneo hilo linakuwa na usalama wa kuwa katika miliki ya Simba.
Achana na Rage na uongozi wake baadaye ukaja utawala wa Rais Evance Aveva na makamu wake Geofrey Nyange ‘Kaburu’ ambao wao wakaanzisha hatua ya ujenzi katika eneo hilo na baadaye hata kununua nyasi za bandia ambazo zimetandazwa sasa katika moja ya kiwanja hicho.
Ikumbukwe hatua ya ujenzi wa viwanja hivi ndio vinavyowatesa viongozi hawa akiwemo pia Zacharia Hans Poppe inawezekana kama isingingekuwa akili ya watu hawa na maamuzi yao magumu inawezekana wasingekuwa na safari za kupanda mahakama ya kisutu ambapo kuna mashtaka yanayowakabili sasa.
Hatua yao ya kuhitaji maendeleo ndio iliwapelekea kukabiliwa na hatua ambayo wako sasa lakini pia tukumbuke mpaka sasa bado watu hao ni watuhumiwa kwa kuwa bado hawajahukumiwa lolote lakini zaidi hata kama watahukumiwa kwa makosa kwa kukiuka utaratibu haitaupoteza Usimba wao.
Wakati tunatambua nguvu ya bodi ya Simba kwa walichofanya katika kumalizia wiwanja hivyo, sidhani kama litakuwa kosa kwa Simba kuwakaribisha viongozi hawa na wote ambao walihusika katika hatua hiyo kukaa katika hafla ya uzinduzi huo na nguvu yao kutambulika kwa uma wa mashabiki na wanachama wa timu hiyo kwa kuwa nao walihusika katika hatua ya mafanikio hayo.
Wakati Simba wakiingia katika historia hiyo nadhani sasa ni wakati muafaka kwa Yanga nao kuanza kuamka katika usingizi na kuamka kuanza harakati mpya za kurudi walikokuwa.
Yanga wanaweza kuwa na tofauti kidogo kwani wao wamewahi kufanya mazoezi katika uwanja wao na hata kucheza mechi katika uwanja wao tofauti na Simba.
Yanga walikuwa na uwanja wao pale Jangwani wa Kaunda ambao ulishawahi kutumika kwa mechi na hata mazoezi na matumizi yake yalikoma miaka hii ya 2000 kama nitakuwa na kumbukumbu sahihi aliyekuwa kocha Torm Saintfiet aliwahi kutumia uwanja huo kwa mazoezi.
Kwa sasa hakuna uwanja tena zaidi ya eneo hilo kujazwa kifusi ikiwa ni hatua ya kuanza ujenzi upya kutokana na eneo hilo kukumbwa na hali ya kujaa maji inaponyesha mvua kubwa.
Yanga sasa wanatakiwa kuanza kutafuta akili mpya na nimeona viongozi wao kupitia kamati ya ujenzi na miundo mbinu tayari wameanza hatua ya kuanza ujenzi katika eneo lao la Kigamboni walilopewa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda.
Hatua hii itakuwa ni chachu katika maendeleo ya soka lakini pia klabu hizi zitakuwa zimeanza kupiga hatua ambayo imechelewa kwa muda mrefu.
0 Comments