Kauli hizo za Kitambi zinachochea uvumi kwamba Aussems harudi tena kikosini humo, kwani akirudi kutakuwa na mvutano mkubwa kati yake na msaidizi wake huy
. Viti vinatarajiwa kuwa vya moto kwenye ofisi za Mwenyekiti wa Simba, Mohammed ‘Mo’ Dewji zilizopo Golden Jubilee Tower leo wakati Bodi ya Klabu hiyo itakapokutana na kocha Patrick Aussems kuamua hatima ya Mbelgiji huyo Msimbazi.
Wakati hayo yakitarajiwa, kocha msaidizi wa Simba, Denis Kitambi, amechochea uvumi kwamba ukurasa wa Aussems umeshafungwa Msimbazi baada ya kuanika udhaifu wa kikosi hicho chini ya bosi wake huyo. Kitambi amebainisha kuwa amekabidhiwa timu ya Simba na Ofisa Mtendaji Mkuu, Senzo Mazingisa na kwamba mazoezi ambazo amekuwa akiwapa wachezaji ni program zake, siyo za Aussems.
Amesema wachezaji chini ya Aussems wamekuwa wakikata pumzi katika kipindi cha pili na kwamba morali ya baadhi yao iko chini kutokana na uendeshaji wa timu ulivyokuwa.
Amesema wachezaji wanaofanya vizuri mazoezini au katika mechi wanazopewa nafasi hutarajia kuendelea kupewa nafasi lakini jambo hilo limekuwa kinyume chini ya Aussems, hali ambao imechangia kushusha morali ya baadhi ya wachezaji.
Kauli hizo za Kitambi zinachochea uvumi kwamba Aussems harudi tena kikosini humo, kwani akirudi kutakuwa na mvutano mkubwa kati yake na msaidizi wake huyo.
Aussems alifungiwa kwa siku tano tangu baada ya mechi yao ya mwisho dhidi ya Ruvu Shooting Jumamosi na leo wakati adhabu hicho inamalizika anatarajiwa kukutana na bodi ya klabu hiyo kujua hatima yake katika kikao kitakachoanza saa 11:00 jioni.Kocha huyo anatakiwa kueleza kwa muda wa siku tatu alipoondoka nchini alikwenda wapi na kwa nini hakufuata utaratibu sahihi wa kuaga kabla ya safari yake hiyo.
Jambo jingine litakalojadiliwa ni kuhusiana na mwenendo wa timu kwa ujumla, kuangalia matokeo, nidhamu, malengo na mambo mengine yote ya kimsingi ambayo yatakuwa yakihusu masuala ya kiufundi tangu Aussems alipoongezewa mkataba wa mwaka mmoja wa kukinoa kikosi hicho.
Mmoja wa vigogo wa Simba, alisema nafasi ya Aussems kuendelea kubaki katika kikosi chao ni ndogo kwani wajumbe wa bodi walikubaliana kuachana naye na kuanza mchakato wa kumtafuta kocha mpya.
“Tulikubaliana kuachana na Aussems ila tulikuwa tunafuata utaratibu ili tusije kuingia matatizoni na CAF, na FIFA,” alisema kigogo huyo (jina lake tunalo).
Mazingisa alipotafutwa kuzungumzia uvumi wa kuachana na Aussems katika kikao chao cha leo, alifunguka mambo kadhaa.
Mazingisa alisema kuachana na kocha kama Aussems, si jambo dogo na pia mchakato wa kutafuta kocha mwingine aliye bora zaidi yake si kitu rahisi, vinahitaji muda na umakini wa hali ya juu.
Mazingisa alisema bado kwanza wapo na Aussems na kama mabadiliko yakifanyika hapo ndio wataanza kueleza mambo mengine kama kuna kocha ambaye ameomba kutaka kuchukua nafasi hiyo au kama kuna wanayemfikiria kumpata.
“Nadhani muda huu tuache kwanza uongozi ufanye kazi yake ya kumsikiliza Aussems, lakini ambacho naelewa hapo katika kuomba nafasi ya kuja kuifundisha Simba baada ya kuwepo kwa taarifa za kuachana na kocha wetu kuna wengi kutoka Ulaya na Afrika ambao wametuma maombi yao kwetu,” alisema.
“Ligi itasimama zaidi ya mwezi mmoja kwa maana hiyo kwa kipindi hiki wala hatuna haraka katika hilo, lakini kama tutampata kocha mpya basi lazima atakuwa na vigezo vya mahitaji ya soka la Afrika, lakini mpaka sasa bado tupo kimya katika hili hadi hapo uamuzi wa mwisho utakapofanyika,” alisema Mazingisa.
Kwa upande wa kocha msaidizi, Denis Kitambi alisema amekabidhiwa timu hiyo kwa zaidi wiki moja sasa.
0 Comments