Windows

KRC Genk Ya Samatta Yapigwa 4-1 Nyumbani UEFA

MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Samatta, usiku wa kuamkia leo, alishindwa kuiongoza vema timu yake ya KRC Genk na kukubali kupoteza mbele ya Liverpool kwa kufungwa mabao 4-1.

 

Katika mchezo huo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya uliochezwa kwenye Uwanja wa Luminus nchini Ubelgiji, Samatta alikuwa nahodha huku akipewa mzigo mkubwa wa kuibeba timu hiyo iliyopo Kundi E.

 

Katika juhudi zake za kuibeba timu yake, dakika ya 27 ya mchezo huo, Samatta akiwa ndani ya eneo la hatari la Liverpool, aliruka kwenda hewani na kuupiga mpira kwa kichwa mbele ya James Milner na mpira kujaa wavuni.

 

Licha ya mpira huo kujaa wavuni, lakini mwamuzi, Slavko Vincic alisema siyo bao kutokana na kabla ya mpira kumfi kia Samatta, mpigaji wa krosi alikuwa ameotea.

 

Uamuzi ya mwamuzi huyo ulisaidiwa na VAR hali ambayo iliwafanya mashabiki wengi wa Genk kupiga kelele kuashiria kutokubaliana naye.

 

Mchezo huo ulioonekana kuwa wa upande mmoja zaidi kutokana na muda mwingi Liverpool kuutawala, Alex OxladeChamberlain alianza kuifungia timu yake ya Liverpool dakika ya pili likiwa ni bao lake la kwanza katika michuano hiyo tangu afunge mara ya mwisho miezi 18 iliyopita katika hatua ya robo fainali dhidi ya Manchester City, Aprili, 2018.

 

Chamberlain aliongeza bao la pili dakika ya 57 akifunga kwa ufundi wa hali ya juu akimalizia pasi ya Roberto Firmino. Sadio Mane akafunga la tatu dakika ya 77 akipokea pasi ya Mohamed Salah, kisha Salah akahitimisha ushindi huo alipofunga bao dakika ya 87 akimalizia pasi ya Mane.

 

Stephen Odey wa Genk, aliipatia timu yake bao la kufutia machozi dakika ya 88.

 

Hivi sasa Genk inaburuza mkia katika Kundi E ikiwa na pointi moja baada ya kucheza mechi tatu. Napoli inaongoza na pointi zake saba, ikifuatiwa na Liverpool yenye sita, huku Salzburg ni ya tatu ikiwa na pointi tatu.

 

Matokeo ya mechi zingine za Ligi ya Mabingwa Ulaya zilizochezwa usiku wa kuamkia leo ni kama ifuatavyo: Salzburg 2-3 Napoli, Inter 2-0 Dortmund, Slavia Prague 1-2 Barcelona, Leipzig 2-1 Zenit St. Petersburg, Benfi ca 2-1 Lyon, Ajax 0-1 Chelsea na Lille 1-1 Valencia

 

The post KRC Genk Ya Samatta Yapigwa 4-1 Nyumbani UEFA appeared first on Global Publishers.


Post a Comment

0 Comments