Windows

Yanga Sasa Mikononi mwa Wasauzi

BAO la kujifunga la kiungo wa Yanga, Abdulaziz Makame limewaondoa Yanga katika Ligi ya Mabingwa Afrika kufuatia kipigo cha mabao 2-1 katika mchezo dhidi ya Zesco United ya Zambia.

 

Yanga iliyofungana 1-1 na Zesco nyumbani kwenye mchezo wa kwanza, itatua kwenye mtoano ya Kombe la Shirikisho Afrika ambako droo yake itachezwa Jumatano ya Oktoba 9 na mechi zitaanza Oktoba 27, mwaka huu.

Huenda ikakutana na Wasauzi.

Katika hatua hiyo, Yanga itacheza mechi moja nyumbani na ugenini na kama ikipata matokeo mazuri itafuzu hatua ya makundi ya Shirikisho itakayoanza Novemba 29.

 

Mpaka juzi jioni, timu zilizokuwa na uhakika wa kukutana na Yanga kwenye hatua hiyo ni Triangle United ya Zimbabwe (iliyowatoa Azam jana), Zanaco ya Zambia, DC Motema Pembe ya DR Congo, Bidvest Wits, TS Galaxy zote za Sauzi na Proline ya Uganda.

 

Katika mchezo wa Yanga jana, ulipigwa kwenye Uwanja wa Levy Mwanawasa hapa Zambia na ulikuwa na upinzani mkali kwa timu zote mbele huku wageni wakipambana kupindua meza kabla ya kujichanganya wenyewe.

 

Zesco inayofundishwa na George Lwandamina imeendeleza rekodi ya kutofungwa katika uwanja wake wa nyumbani kwenye michuano ya kimataifa kufuatia ushindi huo uliowapeleka kwenye hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa ambako kuna mkwanja mnene.

 

Licha ya Yanga kucheza kwa utulivu mkubwa kwenye mchezo huo lakini walikosa makali ya kutosha katika safu ya ushambuliaji huku ikiruhusu mashambulizi mengi langoni kwao kabla ya mshambuliaji Mkenya, Jesse Were kuifungia Zesco bao la kuongoza katika dakika ya 24 baada ya kuunganisha kwa kichwa krosi ya Winston Kalengo.

 

Bao hilo liliwaibua Yanga ambao walianza kulisakama lango la Zesco kabla ya kupata kona dakika ya 29 iliyopigwa na Patrick Sibomana, beki Lamine Moro akamwekea Makame ambaye alipiga shuti kali likapanguliwa na kipa wa Zesco na mpira kumkuta, Sadney Urikhob ambaye alifunga bao la kusawazisha katika dakika ya 30.

 

Hadi timu hizo zinakwenda mapumziko matokeo yalikuwa ni bao 1-1, kipindi cha pili Zesco walianza kwa mzuka wa aina yake na kukosa bao katika dakika ya 58 kwa mpira wa tiktak wa Kalengo na shuti lake kutoka nje.

 

Licha ya Yanga kucheza kwa kujiamini na kujilinda, Zesco waliendelea kuwa moto kutokana na kutengeneza nafasi nyingi za mabao ambazo walishindwa kuzitumia kabla ya Were kukosa bao tena kwa shuti lake kupanguliwa katika dakika ya 68 na kuwa kona ambapo Yanga walikoswa tena kufungwa katika dakika ya 72.

 

Dakika moja baadae, Patrick Sibomana alikosa bao kabla ya Makame kujifunga katika dakika ya 78 wakati alipokuwa akiokoa mpira wa krosi ya chini iliokuwa imepigwa na Were.

 

Bao hilo ambalo liling’ang’ania liliwashusha morali wachezaji wa Yanga ingawa Kocha Mwinyi Zahera aliwasisitiza ‘pambaneni’ lakini meza ilishapinduliwa na wenyeji. Kikosi cha Yanga; Metacha, Ally Ally, Sonso, Moro,Yondani, Mak ame,Kaseke,Feitoto ,Sadney,Tshishimbi na Sibomana.

The post Yanga Sasa Mikononi mwa Wasauzi appeared first on Global Publishers.


Post a Comment

0 Comments