Windows

FURSA LUKUKI KWA WATANZANIA KATIKA KONGAMANO LA BIASHARA KATI YA TANZANIA, UGANDA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na mgeni wake Rais wa Uganda Mheshimiwa Yoweri Museveni kabla ya kuanza mazungumzo yao Chato mkoani Geita mapema Julai 2019. PICHA NA IKULU.

Na Mwandishi Wetu.

MTANZANIA mwenzangu, najua unajua kuwa siku za karibuni nchi za Tanzania na Uganda zinatarajia kufanya Kongamano la kibiashara la pamoja ambalo litakuwa ni mara ya kwanza kufanyika nchini kwetu.

Kwa kukumbusha tu, kongamano hilo linatarajia kufanyika kuanzia Septemba 6 hadi Septemba 7 mwaka huu katika ukumbi wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.

Kongamano hilo baina ya Tanzania na Uganda linatarajia kuwashirikisha wafanyabiashara wa nchi hizo.

Kongamano hilo kwa namna moja au nyingine itakuwa fursa nzuri kwa wafanyabiashara wa nchi hizo kubadilisha uzoefu wa kibiashara na namna nzuri ya kuendelea kushirikiana kwa maslahi ya pande zote mbili.

Serikali ya Awamu ya Tano chini ya utawala wa Rais mzalendo na mwenye upendo kwa nchi Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na mambo mengine ameweka msingi imara katika kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa nchini zinapata soko kwenye nchi nyingine zikiwemo za Afrika Mashariki.

Kauli mbiu ya Tanzania ya viwanda ambayo imekuwa ikihimizwa na Rais wetu imekuwa chachu kwa Watanzania kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa viwanda sambamba na utengenezaji wa bidhaa zenye ubora ambazo zinaweza kushindana kwenye soko la Dunia, Afrika na Afrika Mashariki kwa ujumla.

Kabla ya kuendelea kuzungumzia umuhimu wa kongamano hilo la kibiashara kati ya Tanzania na Uganda naomba kutumia walau dakika moja ama mbili kutoa pongezi zangu za dhati kwa Rais Dk. Magufuli kwa namna ambavyo ameamua kufungua milango ya kuzikaribisha nchi mbalimbali kuja nchi kuwekeza.

Kwa upendo mkubwa kwa nchi yake, amehakikisha anaweka mkazo katika ujenzi wa miundombinu ya uwekezaji na kibiashara na matokeo yake muamko kwa watanzania katika kuwekeza na kufanyabishara umekuwa mkubwa na wenye tija. Hongera Rais wetu kwa kazi nzuri ambayo unaifanya kwa maendeleo ya nchi yetu.

Hata hivyo kupitia kongamano la biashara ambalo linahusisha nchi hizo mbili, ni wazi Tanzania itatumia nafasi hiyo kama fursa ya kutangaza bidhaa zake na wakati huo huo Uganda nayo itaonesha bidhaa zake.

Ni kongamano ambalo kwangu naliona limekuja wakati muafaka hasa kwa kuzingatia chini ya Rais Magufuli nchi yetu imekuwa na mazingira mazuri ya kibiashara. Ni wakati muafaka kwa nchi zote mbili kutumia maonesho hayo kujengeana ujuzi katika utengenezaji wa bidhaa bora na utafutaji masoko.

Pamoja na mambo mengine kupitia kongamano hilo la kibiashara itakuwa sehemu sahihi ya kuweka mbinu na mikakati itakayofanikisha kuongeza thamani kwa bidhaa zinazotokana na mazao.Sina shaka na hilo hata kidogo na ukweli kwa Tanzania imedhamiria kuongeza thamani kwa bidhaa za mazao.

Katika maisha ya kawaida najua unaweza kujiuliza hivi , je Tanzania tunauza nini zaidi kwa nchi ya Uganda? Jibu vyovyote lakini hili ambalo nitakueleza ni muhimu
zaidi. Iko hivi mpaka sasa Tanzania inauza bidhaa za mazao na bidhaa za viwandani nchini Uganda.

Takwimu zilizopo zinaonesha kwa kipindi cha miaka miwili iliyopita Tanzania imeweza kuuza bidhaa za mazao ya chakula na viwandani zenye thamani ya Sh. bilioni 300 kutoka Sh. bilioni 100. Hilo ni ongezeko mara mbili zaidi ya fedha zilizopatikana huko nyuma.

Ninaposema Rais Magufuli ameweka mazingira mazuri ya kibiashara naaminisha na takwimu zinaeleza wazi namna ambavyo nchi yetu ilivyoweka mazingira mazuri katika sekta ya biashara na viwanda.

Nikiri kwa namna ambavyo Tanzania unauza bidhaa zake nchini Uganda na kuingiza kiasi hicho cha fedha, kongamano litakalofanyika nchini litaongeza wigo zaidi wa kibiashara.

Hata hivyo kutokana na umuhimu wa kongamano hilo la kibiashara, Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara imejipanga vema kuhakikisha kongamano hilo linakuwa na tija na ushiriki wa Watanzania unakuwa mkubwa zaidi.

Nakumbuka wakati anazungumzia kongamano hilo Waziri wa Viwanda na Biashara Waziri wa Viwanda na Biashara Innocent Bashungwa amesema kongamano hilo litasaidia kuweka mazingira wezeshi ya kuongeza wigo wa kujenga viwanda zaidi nchini hasa vya usindikaji wa mazao ili kuongeza thamani ya mazao hayo.

Naomba nitoe rai kwa wafanyabishara na wawekezaji na wote wanaojihusisha na sekta ya biashara waliopo nchini Tanzania kuhakikisha wanashiriki kikamilifu na kwa vitendo katika kongamano hilo. Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Magufuli imejikita katika msingi wa kufanya kazi kwa bidiii.

Hivyo kwa wafanyabiashara kupitia kongamano hilo wataendelea kunoa vichwa ili kujiimarisha zaidi kibiashara ana kiuwekezaji kwa maslahi ya nchi yetu na watu wake kwa ujumla. Nihitimishe kwa kukumbusha tena kongamano la kibiashara kati ya Tanzania na Uganda litafanyika Septemba 6 na Septemba 7 mwaka huu. Sote tushiriki bila kukosa.


Post a Comment

0 Comments