Windows

Wizara ya afya kudhibiti kifua Kikuu Magereza


Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto kupitia Mpango wa Taifa wa kudhibiti kifua kikuu na Ukoma kwa kushirikiana na Jeshi la Magereza nchini wanaanza afua ya ufuatiliaji wa kutathimini hali ya huduma za kutokomeza kifua kikuu katika magereza nchini.

Hayo yamesemwa na Kamishna wa Sheria na Uendeshaji wa Jeshi la Magereza (CP) Owesu Ngalama wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa maofisa wa jeshi hilo yanayofanyika kwenye bwalo la magereza ukonga jijini Dar es Salaam.

CP Ngalama alisema kuwa afua hiyo itasaidia jeshi la magereza kuweza kubaini hali ya TB kwenye magereza kwani wanaoingia kwenye magereza ni wana jamii hivyo itasaidia kubaini ugonjwa huo kwa wafungwa na kwa jamii kwa ujumla

“Ugonjwa huu unaambukizwa kwa hewa hivyo kwa tathimini hii itasaidia kuleta utaalam mkubwa kwa wataalam wetu wa tiba waliopo kwenye jeshi kwani hali ya TB sio kubwa kwenye magereza ila lengo ni kuhakikisha hakuna maambukizi makubwa kwani wafungwa wanaingia na kutoka,”alisema CP Ngalama

Aidha,ameishukuru wizara ya afya kwa kuendelea kushirikiana nao kwa muda mrefu hususan kwenye utoaji huduma za afya ikiwemo utoaji wa dawa,vifaa na vifaa tiba pamoja na masuala ya lishe kwenye vituo vya afya vilivyopo kwenye magereza nchini.

Naye Meneja Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Kifua Kikuu na Ukoma (NTLP) kutoka Wizara ya Afya Dkt. Beatrice Mutayoba alisema ugonjwa wa Kifua Kikuu bado ni jangwa kwani bado kuna takribani watu laki moja na elfu hamsini na nne wanakadiriwa kuugua kifua kikuu kila mwaka na inakadiriwa vifo elfu ishirini na saba kila mwaka nchini.

Dkt. Mutayoba alisema kifua kikuu kinaweza kumpata mtu yeyote kwani maambukizi yake ni ya njia ya hewa hivyo yapo makundi hatarishi zaidi ikiwemo magereza hivyo wanaweka jitihada zaidi kuyafikia makundi hayo ili kutokomeza kifua kikuu ifikapo 2030.

“Kama nchi tumepiga hatua kubwa sana kutokomeza ugonjwa huu hivyo tunaongeza juhudi zaidi kwenye makundi hatarishi ikiwemo magereza,migodini,wavuvi ili kuwafikia kwa karibu na kuhakikisha tunapunguza maambukizi ndani ya magereza na maeneo haya”.Alisisitiza

Hata hivyo alisema mkakati wa kudhibiti kifua kikuu upo kwa wananchi wote hivyo kama mpango wanaendelea kutoa elimu kwa watanzania wote mara waonapo dalili waende kwenye vituo vya afya kwani wizara ya afya inatoa dawa,vipimo na huduma za kifua kikuu bila malipo kwenye vituo vya kutolea huduma za afya.

“Magerezani tunaweza utaratibu kwa wanaoingia kuwe na taratibu za uchunguzi ili anapokutwa na kifua kikuu waanze matibabu kwani unapoanza matibabu ndani ya wiki mbili huwezi kuambukiza wengine,” alisema Dkt. Mutayoba

Mikoa kumi na tano itakayoanza na utekelezaji huo ni pamoja na Dar es salaam, Dodoma, Iringa, Kagera, Kilimanjaro, lindi, Mbeya, Morogoro, Mtwara, Mwanza, Pwani, Shinyanga, Singida, Tabora na Tanga.



Post a Comment

0 Comments