Windows

Watanzania tumeamua na uwezo tunao - Rais Magufuli


Rais wa Tanzania, Dkt. John Magufuli amesema Tanzania imeamua na ina uwezo mkubwa wa kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo nchini pasipo  kutegemea fedha zenye masharti zinazotolewa kutoka kwa wafadhili na wadau wa kimataifa wa maendeleo.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Jengo la 3 la Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam, Rais Magufuli alisema uzinduzi wa Jengo la Uwanja huo ni ushahidi wa wazi wa usimamizi na nidhamu ya matumizi ya fedha za Serikali zinazotokana na kodi ya wananchi.

Aliongeza Jengo la Uwanja huo limejengwa kwa asilimia 100 kutokana na kodi za Watanzania, na hivyo kuiagiza Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano pamoja na Wakala wa Barabara Nchini (TANROAD) kusimamia vyema miundombinu ya Uwanja huo kwa kuhakikisha kuwa inatunzwa ili kuakisi vyema taswira ya Jiji la Dar es Salaam na Watanzania kwa ujumla.

Kwa mujibu wa Rais Magufuli alisema jengo hilo litakalokuwa na uwezo wa kuhudumia jumla ya abiria Milioni 6 kwa mwaka limeigharimu Serikali kiasi cha Tsh Bilioni 722 ambazo ni fedha zilizotolewa na Serikali, limeweza kuifanya Serikali kuaminika na kuwa na udhubutu wa kutekeleza miradi ya Maendeleo kupitia fedha za ndani.

“Ipo miradi mingi ya Maendeleo tunayoisimamia kwa fedha zetu za ndani ikiwemo Ujenzi wa reli ya kisasa, mradi wa kufua umeme Mto Rufiji, Barabara za Juu Ubungo, Daraja la Kigongo-Busisi, Daraja la Salender, Ujenzi na ukarabati wa Viwanja vya ndege 15, kujenga rada 4 katika Viwanja vya Ndege vya Dar Salaam, Mwanza, Mbeya na Kilimanjaro, huu ni ushahidi wa usimamizi imara wa fedha zetu za ndani” alisema Rais Magufuli.

Aidha Rais Magufuli alisema kuwa Serikali itaendelea kuimarisha miundombinu ya sekta ya anga nchini, kwa kuwa sekta hiyo imekuwa kiungo muhimu katika maendeleo ya sekta ya Utalii, kwani kila siku takribani watu Milioni 12 duniani hutumia usafiri wa anga kutokana na kuwa njia ya haraka na ya uhakika kwa ajili ya usafirishaji wa abiria na mizigo.

Post a Comment

0 Comments