DAR ES SALAAM: WAKATI ikiaminika kwamba msanii Nasibu Abdul ‘Mondi’ ndiye mwenye ukwasi wa kutisha Bongo, Ijumaa limenasa utajiri wa kushtua anaomiliki msanii wa Bongo Fleva, Seif Shabani ‘Matonya’.
UBUYU MEZANI
Awali, Ijumaa liling’atwa sikio kuwa, jamaa huyo ambaye amekuwa kimya kidogo kwenye muziki ana utajiri wa kutosha licha ya watu wengi kuamini kwamba wasanii wa kizazi cha kina Mondi ndio wenye mafanikio makubwa.
“Watu hawajui tu, kuna watu wana mkwanja kama wote sema tu hawapendi kuzungumza sana au hawapo kwenye vyombo vya habari sana, Matonya anamiliki viwanja, magari na majumba ya kifahari,” kilisema chanzo makini.
ORODHA KAMILI
Chanzo hicho kilienda mbele zaidi kwa kutaja orodha kamili ya ukwasi alionao msanii huyo aliyewahi kutamba na wimbo Anita.
“Ana nyumba Dege Beach Kigamboni ambayo ni nyumba ya biashara na nyumba nyingine ipo Madale. “Ipo nyingine anayoishi ambayo ipo Bahari Beach, nyingine mbili ziko Lushoto –Tanga ambapo moja ya biashara na nyingine anaishi mama yake.
“Mbali na hizo pia kuna nyingine amejenga Nairobi maeneo ya Kitengela.”
MAGARI SASA… Kikizungumzia upande wa magari ya kifahari, chanzo hicho kilisema anamiliki Toyota Harrier (New Model), Toyota Mark X na Toyota Brevis.
WATU WAHOJI NI MUZIKI TU?
Chanzo hicho kilisema watu wengi wamekuwa wakihoji kuhusu utajiri huo wa Matonya kama unatokana na muziki tu au kuna vyanzo vingine vya mapato.
“Wengi wanahoji sana lakini ukweli ni kwamba mimi Matonya ni mtu wangu, najua alipambana sana kipindi cha nyuma wakati anawika, akawekeza kwenye biashara zake lakini nyinyi mnaweza kumuuliza yeye mwenyewe,” kilisema chanzo hicho.
Ijumaa liliingia mzigoni na kujiridhisha kwa kupata baadhi ya mijengo anayomiliki msanii huyo (moja wapo itazame ukurasa wa mbele) pamoja na magari yake.
IJUMAA NA MATONYA
Ili kuweza kupata ukweli zaidi wa ukwasi huo, Ijumaa lilimvutia waya Matonya ambaye alikiri kumiliki utajiri huo na kueleza kuwa umetokana na shughuli zake za muziki pamoja na biashara ya magari.
“Muziki umeniingizia kipato, nina nyumba za kutosha na magari kadhaa, hilo siwezi kuficha. Mafanikio hayo yametokana na muziki lakini pia biashara yangu ya magari.
Ninanunua na kuuza magari Bongo na Kenya na hiyo ndiyo biashara ambayo nimeifanya kwa muda mrefu,” alisema Matonya.
KUHUSU UKIMYA KWENYE GEMU…
Aidha, Matonya alisema kuhusu ukimya wake kwenye gemu ilikuwa kujikita zaidi kwenye biashara lakini pia ndio aina ya maisha yake kwani hukaa muda mrefu bila kuachia ngoma.
“Natumia muda mrefu kidogo kufikiri na ndio maana unaona hata nyimbo zangu huwa zinaishi. Angalia wimbo kama vile Vailet jinsi ulivyoshika. Ni miongoni mwa nyimbo ambazo zinaishi sababu ya kutulia muda mrefu kutunga kitu kizuri,” alisema Matonya.
Alisema hata hivyo haimaanishi ameacha muziki bali tayari ana albamu ambayo anakwenda kuiachia hivi karibuni.
“Nina albamu mpya ambayo natarajia kuitoa mwaka huu ambayo nilikuwa nasubiria masoko yakae vizuri na nitaiuza kwenye mitandao, nina uhakika itafanya vizuri. Kuna nyimbo kali kama Siyo Freshi ambayo nimefanya na Nai Boy na mwingine unaitwa Pagawa na Pilipili ambao nimefanya na Malkia Careen.
Matonya aliwataka mashabiki wake kukaa mkao wa kula kwani albamu hiyo imesheheni nyimbo kali na kama kawaida yake hatawaangusha. Matonya ambaye yupo Bongo Flevani tangu mwanazoni mwa miaka ya 2000, amefanya ngoma kali zilizotikisa ulimwengu wa burudani ikiwemo Uaminifu, Dunia Mapito, Siamini, Tax Bubu na Mrembo.
Stori: NEEMA ADRIAN, IJUMAA
The post Utajiri wa Matonya Washtua, Kuna Nini Nyuma Yake? – Video appeared first on Global Publishers.
0 Comments