Windows

Tutawapiga kwao

KOCHA Mwinyi Zahera hakupendezwa na kitendo cha vijana wake kuruhusu bao wakati wakivaana na Township Rollers ya Botswana, lakini akawataka mashabiki wa Yanga kutulia akiwaahidi wanaenda kuwapiga wapinzani wao kwao wiki mbili zijazo.
Zahera alisema makosa ya vijana wake yamewagharimu na kutoka sare ya 1-1 dhidi ya wageni wao kwenye mechi ya kwanza ya raundi ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini akawahakikisha Wanayanga kwamba wanaenda kumaliza kazi ugenini.
“Katika michuano hii ya Afrika, ukicheza nyumbani hutakiwi kuruhusu kufungwa bao, lakini imetokea na wenzetu wamepata, lakini bado tuna mechi ya marudiano ugenini nasi tunaenda kupambana kupata mabao zaidi ili kusonga mbele,” alisema Zahera.
Katika mechi hiyo iliyochezwa kuanzia saa 12 jioni, Yanga ikirejea kwenye michuano ya kimataifa tangu misimu miwili iliyopita, ilishtukizwa kwa bao la mapema la dakika ya nane kupitia kwa Phenyo Serameng aliyefumua shuti kali la mguu wa kushoto.
Mkwaju huo murua ulimuacha kipa Metacha Mnata aliyekuwa akiidakia timu hiyo kwa mara ya kwanza kwenye mechi ya mashindano baada ya Farouk Shikalo kushindwa kuipata leseni yake mapema, iliwakata stimu mashabiki waliojitokeza uwanjani.
Yanga walionekana kucheza kwa presha huku wakipiga pasi ambazo hazikufikia hata tano kabla ya mpira kuchukuliwa na wapinzani, walicharuka kutaka kurudisha bao hilo na dakika moja tu baada ya kufungwa Sadney Urikhob alipiga pasi ndefu ndani ya boksi lakini Patrick Sibomana alishindwa kuunganisha kwa mguu.
Dakika 30 Juma Balinya alipiga krosi iliyokutana na Mapinduzi Balama alipiga kichwa (diving header) na mpira ulimgonga mkononi beki wa Township Rollers na kuwa penalti iliyopigwa na Sibomana, lakini kipa wa Township, Wagare Dikago aliokoa penalti hiyo.
Kukoswa kwa penalti hiyo kuliwanyong’onyesha mashabiki wa Yanga waliokuwa na kiu ya kutaka kuona chama lao linatoka na ushindi nyumbani ili kulipa kisasi cha kipigo cha mabao 2-1 ilichopewa na Rollers mwaka jana kwenye mechi ya michuano hiyo. Katika kipindi cha pili Yanga waliingia kwa spidi ya kuonyesha kuhitaji kupata goli la kusawazisha, walikuwa wakipigiana pasi za haraka haraka na kuingia ndani ya boksi lakini kipa wa Rollers, Wagare Dikago alikuwa mwiba wa kuokoa michomo.
Dakika 65 Yanga walifanya mabadiliko ya kumtoa Juma Balinya na kuingia Issa Bigirimana kwenda kuongeza nguvu katika eneo la ushambuliaji, wakati huo huo Rollers walimtoa Serameng na kuingia Arnold Mampori na dakika 77 Yanga walimtoa Mapinduzi Balama na kuingia Mrisho Ngassa.
Dakika 86 Yanga walisawazisha kwa mkwaju wa penalti iliyopigwa na Sibomana, penalti iliyotokana na Sibomana kupiga krosi ndani ya 18 na beki wa Rollers aliunawa mpira.
Kwa matokeo hayo, Yanga italazimika kupata sare yoyote ya mabao kuanzia mawili ama ushindi ili kuing’oa timu hiyo katika mechi ya marudiano wiki mbili zijazo kama inataka kufuzu raundi ya kwanza. Mapema kabla ya kuanza mchezo Yanga walikuwa wamejifunga vitambaa vyeusi wakihani msiba wa raia waliopoteza maisha kwa ajali ya moto mkoani Morogoro.

Post a Comment

0 Comments