KLABU za Simba na Azam FC ambazo wikiendi zilikuwa kwenye majukumu ya kimataifa zimeanza kuwachanganya mabosi wa Chama cha Soka Mkoa wa Iringa kwa ajili ya maandalizi ya pambano lao la Ngao ya Jamii ya kuzindua msimu mpya wa Ligi Kuu Bara.
Simba ilikuwa Msumbiji katika mechi yake ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya UD Songo wakati Azam leo Jumapili itashuka ugenini kule Ethiopia kupepetana na wenyeji wao, Fesil Kanema katika mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Baada ya mechi hizo timu hizo zitasafiri hadi Iringa kuumana kwenye mechi ya Ngao ya Jamii itakayopigwa Uwanja wa Samora na mabosi wa soka wa mkoa huo, wamefunguka namna wanavyokimbizana kwa sasa kuweka mambo sawa kabla ya klabu hizo kuumana.
Mwenyekiti wa chama cha soka Mkoa wa Iringa (IRFA), Cyprian Kuyava alisema mechi hiyo ni fursa ya kipekee kwa mkoa huo kwani ni ugeni mkubwa utakaowapa vijana wao vipato kwa kazi mbalimbali watakazofanya na hivyo wanapambana kuona kila kitu kinaenda poa.
“Ni mara yetu ya kwanza kuandaa mchezo wa Ngao ya Jamii, hivyo tumefanya maandalizi mazuri ya kuhakikisha mabosi wetu wa juu wanafurahishwa, ili tuweze kupata nafasi wakati mwingine,” alisema Kuyava.
Aliongeza fursa walizokuwa wakizipata wajasiliamali wakati wa michezo ya Ligi Kuu, na sasa watanufaika zaidi kutokana na kuzihusisha timu kubwaMsimu uliopita Simba na Azam zimekutana mara nne, kwenye Ligi Kuu michezo miwili huku Simba ikishinda mchezo mmoja 3-1 na suluhu moja, Kagame na Kombe la Mapinduzi Azam FC ikishinda michezo yote miwili kwa mabao 2-1.
Ngao ya Jamii huwakutanisha mabingwa wa Ligi Kuu na wa Kombe la FA na msimu uliopita Simba iliitambia Mtibwa Sugar kwa mabao 2-1 katika mechi iliyopigwa Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
Mechi za Ngao ya Jamii zilianzishwa kwa mara ya kwanza mwaka 2001 kabla ya kusitishwa kwa miaka kadhaa na kurejea tena kuanzia mwaka 2009.
Tangu kuanzishwa kwake Simba na Yanga ndizo zinaongoza kwa kutwaa mara nyingi taji hilo, Simba ikibeba mara sita na Yanga mara tano, huku Azam FC na Mtibwa Sugar zikibeba mara moja moja kila mmoja.
0 Comments