KIKOSI cha Simba, kinatarajia kuendelea na mazoezi leo kujiandaa na mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Azam, ukiwa ni kiashiria cha ufunguzi wa msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Mbali ya mchezo huo utakaochezwa Agosti 17, mwaka huu, kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, mazoezi hayo pia ni maandalizi ya kipute cha marudiano cha Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya UD Songo ya Msumbiji.
Katika mchezo wa awali uliochezwa kwenye Uwanja wa Estadio da HCB, jijini Beira, Simba iliwabana UD Songo na kutoka nao suluhu.
Akizungumza na MTANZANIA jana, kocha wa viungo wa timu ya Simba, Aden Zrane, alisema waliwapa wachezaji wao mapumziko ya siku moja kwa sababu ya Sikukuu na leo wataendelea na mazoezi.
“Tulivyorejea, tulifanya mazoezi katika viwanja vya Gymkhana, lakini leo (jana), tuliwapa mapumziko wachezaji na baada ya hapo, tutaendelea na mazoezi kujiandaa na michezo inayotukabili mbele yetu,” alisema.
Alisema wanahitaji kuwaweka fiti zaidi wachezaji wao, kutokana na kukabiliwa na mechi ngumu na zenye ushindani.
Simba ndio mabingwa watetezi wa Ngao ya Jamii, waliyoitwaa msimu uliopita kwa kuifunga Mtibwa Sugar mabao 2-1, kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
Simba imepania kuendeleza ubabe wake msimu huu katika kila michuano watakayoshiriki, kuanzia Ligi Kuu Bara, Ligi ya Mabingwa Afrika na mingineyo.
0 Comments