Windows

Sheikh Mkuu Manyara awataka Waislamu kuwaombea majeruhi wa ajali ya Moto


Na John Walter, Manyara

Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Sheikh Mohammed Kadidi  ametoa salama za rambirambi kwa Rais John Magufuli na Watanzania wote kwa kupoteza wapendwa wao katika ajali ya moto iliyotokea wiki iliyopita mkoani Morogoro na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 70 hadi sasa huku wengine wakiwa Mahututi wakiendelea kupatiwa matibabu Hospitali ya Muhimbili na Mororgoro.


"Mkoa wa Manyara tumepokea kwa masikitiko taarifa za msiba huo ulioacha yatima wengi,wajane na wagane ,tunawaombea faraja wote waliopoteza jamaa na ndugu zao. Natoa pole kwa Rais Magufuli kwa kuondokewa na nguvu kazi ya Taifa, ," amesema Sheikh Kadidi.

Akizungumza na mamia ya waumini wa dini ya Kiislamu waliohudhuria baraza la Idd Al-Adha iliyofanyika Agosti 12 katika uwanja wa Kawaraa mjini Babati amewahimiza kuendelea kuwaombea kwa Mwenyezi Mungu Majeruhi ili waweze kupona na kurejea katika hali zao za kawaida.

Amewaagiza viongozi wa Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata) mkoani Manyara  kuzidi kushirikiana pale panapotokea jambo linalohitaji mchango ili kuzidi kustawi kiimani kama alivyokuwa akijitolea Mtume Mohamad .

Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Babati ambaye alikuwa mgeni rasmi katika Baraza hilo,amewapongeza viongozi wa dini  kwa kuendelea kuunga mkono jitihada zinazofanywa na serikali katika Nyanja mbalimbali za Maendeleo pamoja na kudumisha amani iliopo.

Katika baraza hilo la Idd ilifanyika Harambee maalum kwa ajili ya kumalizia deni la shilingi milioni tano (5,000,000) za gari la ofisi litakalokuwa likitoa huduma kwenye wilaya tano za mkoa wa Manyara.

Kwenye  harambee hiyo zaidi ya shilingi milioni 3 zilipatikana huku  Mbunge  wa Jimbo la Babati mjini Paulina Gekul akichangia shilingi Milioni moja.

Post a Comment

0 Comments