Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) Awamu ya Saba imedhamiria kuendeleza sekta ya kilimo kwa gharama yoyote ile kutokana na umuhimu wa sekta hiyo.
Dk Shein aliyasema hayo katika ufunguzi wa Maonyesho ya Nane Nane yaliyofanyika Langoni, Wilaya ya Magharibi Mkoa wa Mjini Magharibi ambayo yalihudhuriwa na viongozi mbali mbali wa vyama vya siasa na serikali akiwamo Makamuwa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd pamoja na wananchi wengine.
Alisema kwa kutekeleza dhamira hio, serikali imechukua mkopo wa Dola za Marekani milioni 59 kutoka Benki ya Exim ya Jamhuri ya Korea za ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji maji katika hekta 1,524 Unguja na Pemba.
Aliyataja mabonde yatakayohusika na mradi huo kuwa ni Makwararani, Mlemele kwa upande wa Pemba na Cheju, Kibokwa, Chaani, Kinyasini na Bumbwisudi kwa Unguja, ambako hivi sasa mkandarasi wa Kampuni ya KOLON kutoka Jamhuri ya Korea tayari ameshaanza ujenzi huo kwa bonde la Chaani na Kinyasini.
Alieleza kuwa lengo kuu ni kuimarisha kilimo cha kisasa kwa kuongeza zao la mpunga nchini na kupunguza kwa kiasi kikubwa kuutegemea mchele kutoka nje ya Zanzibar, huku akiiagiza Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi kuongeza maduka wanayouza mchele ambao unazalishwa Zanzibar.
Aliongeza kuwa serikali imetenga Dola za Marekani milioni 20, ambazo dola milioni 10 kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na milioni 10 ni msaada wa Mfuko wa Khalifa kutoka Umoja wa Nchi za Falme za Kiarabu (UAE) kwa kipindi cha miaka mitano kutoka 2019 hadi 2024.
Alisisitiza kuwa katika mwaka wa fedha wa 2019/2020, bajeti ya kilimo imeongezeka hadi kufikia Sh bilioni 88.17 kutoka Sh bilioni 62.62 zilizoingizwa mwaka 2018/2019 ambapo ongezeko hilo ni sawa na asilimia 29 ambalo ni kubwa kwa kipindi cha mwaka mmoja.
Aidha, alisema sekta ya kilimo ambayo kama inavyoeleweka kuwa inajumuisha mazao, mifugo, uvuvi, misitu na maliasili zisizorejesheka inaendelea kuwa ni tegemeo kubwa kwa uchumi wa Zanzibar na inachangia moja kwa moja kwa wananchi katika kujikimu maisha yao.
Rais Shein alisema kaulimbiu ya mwaka huu isemayo “Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa Ukuaji wa Uchumi wa Nchi Yetu” inakwenda sambamba na mipango na mikakati ya Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu ya mwaka 2015-2020, MKUZA III na Malengo Makuu ya Maendeleo Endelevu.
Awali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi, Mariam Abdalla Sadalla alieleza kuwa maonesho hayo ya pili ya kilimo yaliyoanza mwaka 2017 yamefanikiwa kwa kiasi kikubwa na na kuwa taasisi 172 zimeshuriki ikilinganishwa na taasisi 83 zilizoshiriki mwaka huo wa 2017.
0 Comments