Licha ya kuwa na faida ya bao la ugenini walilolipata katika sare ya 1-1 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Jumamosi iliyopita, kocha Mkuu wa Township Rollers, Tomas Trucha mzaliwa wa Jamhuri ya Czech, ameshindwa kujiamini kwa asilimia zote kuibuka na ushindi ama kulinda matokeo hayo ili kuweza kusonga mbele, imefahamika.
Kutokana na matokeo hayo, mechi ya marudiano itakayopigwa Jumamosi ya Agosti 24, mwaka huu katika Uwanja wa Taifa mjini Gaborone, Botswana, Yanga itakuwa ikihitaji ushindi ama sare ya kuanzia mabao mawili ili kusonga mbele kwenye michuano hiyo inayoongoza kwa utajiri kwa ngazi ya klabu barani Afrika.
Hata hivyo, kuelekea mechi hiyo ya marudiano, Kocha Mkuu wa Township Rollers, Trucha amesema bado wana kazi kubwa ya kufanya mbele ya Yanga baada ya kuruhusu wenyeji wao kusawazisha na kufanya matokeo kuwa bao 1-1 katika Uwanja wa Taifa.
Township Rollers ambayo ilipata bao dakika ya saba tu tangu mechi hiyo ilipoanza Jumamosi iliyopita, kabla ya Ptrick Sibomana kuisawazishia Yanga kwa mkwaju wa penalti dakika ya 86, sasa itahitaji ushindi ama sare tasa ili kusonga katika michuano hiyo ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
"Pamoja na kwamba sina hofu kubwa sana, tunapaswa kujipanga vema kwa kuwa tunacheza na timu ambayo ina wachezaji wenye kiu ya kupata matokeo, hivyo hatupaswi kuwabeza hata tukiwa uwanja wa nyumbani.
"Tayari tumefahamu namna wapinzani wetu wanavyocheza na mbinu wanazotumia, si watu wa kukata tamaa, licha ya kwamba tuliwabana mwanzo kwa kuwafunga mapema, waliendelea kutuandama na mwisho wa siku wakapata bao," Trucha alifunguka.
Hata hivyo, Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera, ambaye atakuwa na mechi mbili za kirafiki dhidi ya Polisi Tanzania itakayopigwa mjini Moshi na FC Leopards ya Kenya itakayopigwa jijini Arusha, lengo likiwa ni kurekebisha makosa aliyoyabaini kabla ya kuwafuata wenyeji wao, Township Rollers, atakachokifanya ni kuhakikisha anaifanyia kazi safu ya ushambuliaji ambayo ilifanya makosa mengi.
"Kuna makosa mengi yaliyofanywa na wachezaji wangu hususan safu ya ushambuliaji huku muunganiko wa timu bado ukionekana haujakaa sawa, tulitarajia kushinda nyumbani, lakini hilo halikuwezekana.
"Tunatambua katika michuano hii ni muhimu kushinda nyumbani, lakini tunaweza kuingiza mabao hata mawili kwao, hasa tukizingatia tuna mechi moja yakutupa tiketi ya kusonga mbele, wao wamepata bao kwetu na sisi tunaweza kufanya hivyo kwao," alisema.
Katika mechi hiyo ya marudiano, Yanga itapaswa kuwa makini hususani kwa nyota aliyeanza kuwaliza dakika ya saba, Phenyo Serameng.
Mshindi wa jumla kati ya Yanga na Township Rollers atakutana na mshindi wa jumla wa mechi kati ya Green Mamba ya Eswatini (zamani Swaziland) na Zesco ya Zambia.
0 Comments