Windows

Pamba SC na mkakati wa kutimiza ndoto iliyoishindwa miaka 20


MIAKA zaidi ya 20 imepita sasa tangu timu ya Pamba ya Mwanza, iliposhuka daraja kutoka Ligi Kuu Tanzania.
Tangu wakati huo hadi hii leo, Pamba ambayo pia ni maarufu kwa jina la TP Lindanda inahaha kuhakikisha inarejea kwenye mikiki mikiki ya Ligi Kuu, lakini mambo bado yanaonekana kuwa magumu.
Timu hiyo ina historia kubwa katika soka la Tanzania na Afrika Mashariki ikiwa ni pamoja na kutoa wachezaji wengi nyota waliowahi kutamba chini.
Juhudi zake za kurejea Ligi Kuu bado hazijafua dafu, ambapo msimu uliopita iliishia kwenye hatua ya mtoano, baada ya kutolewa na Kagera Sugar.
Hamu ya kukipiga tena Ligi Kuu imezidi kuongezeka, ambapo msimu ujao hamasa imeongezeka maradufu kwani tayari imeweka mikakati kibao ya kuhakikisha kila jambo linakwenda barabara.
Kwa mujibu wa Makamu Mwenyekiti wa Pamba , Aleem Alibhai anasema, klabu yao iliyoanzishwa mwaka 1968 ikiwa na miaka 51, inalenga kurejea upya kwenye chati na mwaka huu wameuchagua kuwa
 wa kimapinduzi kwa kuanza na kuipandisha Ligi Kuu.
“Juhudi hizi ni kurudisha heshima na kuendelea kuifanya klabu yetu kuandika historia na kurejea Ligi Kuu, baada ya msimu uliopita kukwama katika hatua ya mtoano,” anasema.
Usajili
Klabu hiyo imefanya usajili wa kishindo kutokana na kuwashusha nyota wazoefu wa Ligi Kuu akiwemo Abasarim Chidebele aliyewahi kutamba na Stand United, Nizar Khalfani aliyewahi kucheza Yanga, Singida United na timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars).
Nizar pia amewahi kucheza soka la kulipwa katika klabu ya Vancouver Whites Capes ya nchini Canada.
Pamba pia imemsajili mlinda mlango wa timu ya taifa ya umri chini ya miaka 17, Crytone Boniphace.
Wengine ni Saad Kipanga kutoka JKT Tanzania, Gaudence Mwaikimba aliyewahi kutamba na timu kadhaa ikiwemo Yanga na Taifa Stars, Salvatory Ntebe kutoka JKU ya Zanzibar wanaoungana na mkongwe Shija Mkina aliyekuwepo hapo tangu msimu uliopita.
Benchi la ufundi
Katika kuhakikisha kila kitu kinakwenda sawa, klabu hiyo imefanya mageuzi makubwa katika benchi lake la ufundi, kwa kuongeza watu wenye uzoefu na wasifu mkubwa.
Uongozi wa Pamba unaamini jopo hilo litaiwezesha klabu yao kufanya vyema Ligi Daraja la Kwanza na hatimaye kupanda Ligi Kuu.
Klabu hiyo kupitia Kamati ya Utendaji, ilimteua Muhibu Kanu kuwa Kocha Mkuu kwa mkataba wa mwaka mmoja.
Pia Hafidh Mamboleo (Yangoo),atakuwa kocha msaidizi, Venance Kazungu, Mratibu na Mshauri wa timu, Philipo Richard atahudumu nafasi ya daktari na mtaalamu wa viungo, Japhari Juma atafanya kazi ya umeneja na Jumanne Marcelo atakayeshughulika na tathmini, nidhamu na takwimu za wachezaji uwanjani.
Mkataba vifaa vya michezo
Pamba iliingia mkataba wa miaka miwili wa udhamini na kampuni ya mavazi ya Chief Empire, kwa ajili ya uzalishaji wa jezi za timu hiyo pamoja na vifaa vingine vya michezo.
Mkataba huo pia utahusu udhamini wa
 jezi za nyumbani, ugenini, na zile za ziada, jezi za mazoezi na vifaa vingine pamoja na jezi zitakazouzwa kwa mashabiki.
Mkataba huo ulisainiwa jijini Mwanza mwishoni mwa Julai, mwaka huu , ikiwa ni utekelezaji wa kanuni mpya zinazozitaka timu za Daraja la Kwanza na Ligi Kuu kuwa na jezi tatu, ugenini, nyumbani na ziada.
Timu ya vijana
Katika kuhakikisha inakuwa na kizazi cha muda mrefu kitakachoibeba kwa miaka ijayo, Pamba iliingia mkataba wa miaka miwili na kituo cha michezo cha Pamoja Sports Center cha Mwanza , kwa ajili ya maendeleo ya soka la vijana hususan walio na umri chini ya miaka 17.
Timu za kituo hicho zitaitwa Pamba SC kwa kipindi cha miaka miwili na watacheza michezo yote ya utang ulizi itakayoihusu Pamba.
Lengo ni kuwaandaa vijana walio na umri chini ya 17 watakaoanza kuonekana msimu ujao hususan kwenye michezo ya Pamba na michuano ya vijana.
“Program hii ya Youth Development inalenga hadi kufikia mwaka 2021, iwe imezalisha wachezaji wazuri ambao ni zao la klabu yetu, tumekubaliana timu yao ya U-17 itaitwa Pamba SC kwa miaka miwili na mauzo ya wachezaji, lakini pia tunataka kuenzi utamaduni wa soka la Pamba lenye kandanda safi na mpira wa chini.
“Vile vile vijana hao watakuwa wanasafiri na klabu yetu kwa mechi za ugenini, wachezaji watano watakaokuwa wanapata mafunzo lakini michezo ya nyumbani watacheza mechi za utangulizi zinazohusu klabu yetu,” anasema Alibhai.
Mshauri benchi la ufundi
Katika kuhakikisha inaendeshwa kisasa na mipango ya benchi la ufundi inakwenda sawa, Klabu ya Pamba ilimteua Amani Josiah kuwa mshauri mkuu wa benchi la ufundi.
Kabla ya uteuzi huo, Amani alikuwa Kocha Msaidizi wa timu ya Biashara United na baadae meneja wa timu hiyo, pia ni miongoni mwa waanzilishi wa Biashara United kabla ya kuwa kocha wake tangu ikiwa daraja la tatu mpaka Ligi Daraja la Kwanza na baadae kupanda Ligi Kuu.
Ushirikishwaji wazee wa Pamba
Wana TP Lindanda wamedhamiria kuirejesha timu yao Ligi Kuu, ambapo sehemu ya mikakati hiyo ni kuwashirikisha kila hatua wachezaji wa zamani na wazee wa timu hiyo, ili kuepuka migogoro na kupata mawazo yatakayoisaidia kusonga mbele.
Alibhai anasema kuwa, kikao cha kamati ya utendaji kilipitisha azimio hilo na kusisitiza kuwa matukio yote yanayoihusu klabu yao lazima wazee na wachezaji wa zamani wa timu hiyo wawepo.
Pia walimpitisha mwenyekiti wa zamani wa klabu hiyo, Miraji Kazimoto na wenzake kuwa wanachama wa heshima ndani ya timu hiyo.

Post a Comment

0 Comments