Windows

Ni mwendo wa kuuliza ‘kituo kinachofuata’?




HAMNA ubishi ‘This is next level’ ni kaulimbiu watakaotumia msimu mpya wa ligi. Ni kaulimbiu ambayo walibuni na kuitumia wakati wakiadhimisha tamasha la SportPesa Simba Week. Na kwa namna yalivyokuwa wanagawa dozi kwa kila timu wanayokutana nayo, mashabiki walikuwa wakisikika wakiuliza ‘kituo kinachofuta?’.

Simba wamepania kuzoa mataji yote msimu huu kutokana na kikosi walichokisajili na kambi waliyoweka nchini Afrika Kusini.

Tusisahau Simba ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara kwa misimu miwili mfululizo na wamedhamiria kulitetea kwa msimu wa tatu ikiwemo kufuzu zaidi ya hatua ya robo fainali Ligi ya Mabingwa Afrika.

Mchezaji kipenzi wa Wanasimba atakayekosekana msimu huu ni straika raia wa Uganda, Emmanuel Okwi, aliyejiunga na Al Ittihad ya jijini Alexandria nchini Misri. Hata hivyo, uongozi wa Simba umefanikisha kumuongeza mkataba straika raia wa Rwanda, Meddie Kagere, na kumsongeshea karibu mafundi wa mipira Francis Kahata, Deo Kanda na Ibrahim Ajib.

Kwa aina ya wachezaji wanaomzunguka Kagere na ukingatia katika kilele cha sherehe za Simba Day alifunga hat-trick, tutarajie akitetea tena Kiatu cha Dhahabu kwa kufunga zaidi ya mabao 23 ya msimu uliopita. Vilevile tusisahau kwenye safu ya ushambuliaji pia yupo nahodha John Bocco naye ana uwezo wa kupachika zaidi ya mabao 16 aliyofunga kwenye ligi msimu uliopita.

Huenda pia Simba wakavunja rekodi ya pointi 93 walizozoa msimu uliopita lakini hiyo itategemea namna gani kocha wao raia wa Ubelgiji, Patrick Aussems, atakavyotumia kikosi chake kipana kupigania mataji yaliyombele yao.

Mataji tunayozungumzia ni Ligi Kuu Bara, Ligi ya Mabingwa Afrika, Kombe la FA (Azam Sports Federation Cup) na Kombe la Mapinduzi. Sio mataji tu, kwa namna umati mkubwa ulivyojitokeza Simba Day, tutarajie wataongoza kuvuna fedha nyingi kwa mapato yanayotokana na viingilio uwanjani.

Msimu uliopita, Simba iliongoza kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa mwezi ikifanya hivyo mara sita kati ya tisa. Kagere alitwaa mara tatu (Agosti, Februari na Mei) wakati Bocco mara mbili (Machi na Aprili) na Okwi akitwaa tuzo ya Oktoba. Aussems naye alitwaa tuzo ya kocha bora wa mwezi mara mbili (Machi na Aprili).

Waliyoingia: Gerson Fraga Viera, Deo Kanda, Beno Kakolanya, Ibrahim Ajib, Miraji Athumani, Tairone Santos da Silva, Sharaf Shiboub, Gadiel Michael, Kennedy Juma, Haruna Shamte, Wilker Henrique da Silva na Francis Kahata.

Waliyoondoka: Deo Munishi, Asante Kwasi, Emmanuel Okwi, James Kotei, Said Mohammed, Mohammed Rashid, Marcel Kaheza, Zana Coulibaly, Emmanuel Mseja, Mohammed Ibrahim, Haruna Niyonzima, Adam Salamba, Nicholas Gyan, Abdul Selemani na Paul Bukaba.

Post a Comment

0 Comments