Windows

Mnaiga ushangiliaji wa Kagere au kiu yake?




MCHEZO wa Ngao ya Jamii unaotarajiwa kuchezwa leo Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kati ya Simba na Azam FC utaashiria kuzinduliwa rasmi pazia la Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2019/20.

Ngao ya Jamii inawakutanisha mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara msimu uliopita dhidi ya washindi wa Kombe la FA yani Azam Sports Federation Cup, Azam FC.

Moja ya vitu vitakavyokumbukwa ambavyo vilichukua taswira kubwa katika soka msimu uliopita ni aina ya ushangiliaji wa straika wa Simba, Meddie Kagere, hususan ya kuziba jicho moja mara baada ya kufunga bao.

Staili ya kuziba jicho moja akitumia kiganja cha mkono wake kwa nyota huyo mzaliwa wa Uganda aliyechukua uraia wa Rwanda iliweza kubamba hata nje ya uwanja ambako mashabiki waliitumia kuashiria kukubaliana na kile anachokifanya.

Hakuna shaka Kagere ni hatari zaidi, na hii inatokana na takwimu zake za ufungaji mabao katika Ligi Kuu Tanzania Bara ambayo inasadikiwa ndiyo ngumu lakini yenye mvuto katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Msimu wa 2017/18, Kagere aliondoka na Kiatu cha Dhahabu Ligi Kuu ya Kenya akiwa na kikosi cha Gor Mahia, na alipojiunga na Simba msimu uliofuata, aliibuka kinara na mabao yake 23.

Katika kuonyesha yeye ni hatari kwenye kucheka na nyavu, Kagere alifunga mabao mengine sita katika Ligi ya Mabingwa Afrika kuanzia hatua ya awali hadi robo fainali.

Umahiri wake huo wa kucheka na nyavu ndio unaoendelea kuchochea umaarufu wake Tanzania na nje ya mipaka. Umaarufu huu ungeweza kumpa jeuri Kagere na kujiona mfalme katika timu yake.

Huenda tulitarajia kumuona Kagere angechelewa kurejea mazoezini, kuzozana na uongozi au kususia kitu fulani kama ambavyo tumesikia na kuona kwa wachezaji wengine wa kigeni ambao wamekuwa na viwango bora katika timu zetu za Tanzania.


Mbali na wageni, hata wenyeji wengi ambao baada ya kupata mafanikio kidogo, tumekuwa tukisikia wakifanya vituko mbalimbali wakati mwingine kugoma, ulevi, kuchelewa kuripoti kambini na aina yoyote ya utovu wa nidhamu, lakini imekuwa kinyume kwa Kagere.

Ni wazi Kagere hajalewa sifa ya umaarufu kutokana na uwezo aliyonayo na badala yake ameonekana kuthamini kile kilichomleta Tanzania.

Tayari Mnyarwanda huyo ameonyesha yupo kikazi zaidi Tanzania na kuna kila dalili ya kuibuka Mfungaji Bora kwa mara ya pili mfululizo baada ya kuonyesha cheche zake siku chache kabla ya kuanza kwa ligi.

Kagere aliweza kuzitikisa nyavu za Power Dynamos ya Zambia mara tatu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam ukiwa ni mchezo wa kirafiki wakati wa maadhimisho ya kilele cha Simba Day.

Hapa ndipo unapojua Kagere yupo Tanzania kutafuta fedha na si vinginevyo kutokana na njaa ya mafanikio aliyonayo. Unaweza kusema mechi ile ni ya kirafiki tu, au ya bonanza, lakini ni baadhi ya vitu vidogo vinavyoongeza thamani ya mchezaji.

Tukumbuke huyu ni mchezaji aliyechangia kuifikisha Simba robo fainali Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita achilia mbali kutetea taji la Ligi Kuu Tanzania Bara.

Swali ambalo nitahitaji majibu yake kutoka kwa wachezaji wetu wazawa, wanachokiiga kutoka kwa Kagere ni maisha yake ya soka au aina ya ushangiliaji wake?

Kama watakuwa wakiigia aina ya ushangiliaji ya kuziba jicho moja na kuona inatosha, basi hawana budi kujua hili hata maisha ya Kagere katika soka yanafaa kuigwa.

Pengine Kagere ni mtu anayejinyima baadhi ya mambo katika maisha yake binafsi, ili kuwa na mwendelezo mzuri katika soka, hivyo na wazawa nao wanapaswa kuiga mfumo wake wa maisha.

Pia, nidhamu katika kazi pamoja na kuthamini kile walichojaaliwa na Mungu ambacho kinawapa riziki ya kila siku.

Wachezaji wa Bongo msikwame kwenye mambo yanayowakandamiza katika maisha yenu ya soka, jifunzeni kwa Kagere. Mtafika mbali.

Post a Comment

0 Comments