Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha amemuagiza Mkurugenzi wa Manispaa ya Bukoba, Morris Limbe kumlipa fedha Mkandarasi anayekarabati shule ya sekondari Bukoba ili aweze kuendelea na kazi na kukamilisha ukarabati huo kwa wakati
Naibu Waziri Ole Nasha ametoa agizo hilo mkoani Kagera wakati wa ziara ya kukagua miradi ya maendeleo ya sekta ya elimu inayotekelezwa mkoani humo, ambapo amesema Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ilishapeleka fedha zote za ukarabati huo kiasi cha shilingi bilioni 1.4 lakini mpaka sasa mkandarasi huyu amelipwa kiasi cha shilingi milioni 32 tu.
“Fedha zilishaletwa zote na wizara shilingi bilioni 1.4 lakini mpaka sasa Mzinga wamelipwa shilingi milioni 32 tu kati ya milioni mia mbili na zaidi walizotakiwa kuwa wamelipwa mpaka sasa, hivyo Mkurugenzi wa manispaa dirisha likifunguliwa hakikisha Mzinga wanapata fedha ambazo wanadai” amesisitiza Ole Nasha.
Ole Nasha amesema ukarabati wa shule hiyo unaoendelea umechelewa kukamilika kwani licha ya fedha hizo kupelekwa mapema mkandarasi amechelewa kuanza kufanya ukarabati huo. Hata hivyo amesema kasi ya ujenzi huo si mbaya kutokana na kuanza mwezi wa tano.
0 Comments