Windows

Kuna usajili laini za chuo na usajili wa Molinga Yanga !


KWA mujibu wa jamhuri ya Instagram, Haji Manara anakubalika Simba kuliko MO Dewji. Kuna swali hapa; kati ya usajili wa laini za simu za chuo na usajili wa Molinga Yanga upi ndio usajili? Tuwemo kijiweni leo hii!


LUQMAN: Daktari Levy siku hizi hatumsikii daktari mwenzako Louis Shika. Huwa anahudhuria vikao vyenu vya madaktari?


LEVY: Sidhani kama una kumbukumbu sawa sawa. Ni juzi tu katangaza kuwadhamini wazee wa Kubwa Kuliko.


LUQMAN: Ooh, amewekeza Shi-ngapi? Ooh sorry, ana followers wangapi Instagram?


LEVY: Huko insta binafsi sifuatilii... Ila ukweli ni kwamba bado jamaa ana pesa. Kaamua kula kimya kimya, anaogopa kudangiwa na totoz sampuli ya Gigy Money.


LUQMAN: Bongo kuwa followers wengi Instagram ndio utajiri. Kama Shika hana wafuasi Insta, huyo hana kitu. Si unaona Haji Manara ana wafuasi zaidi ya Milioni 1.4 amekuwa heavyweight mpaka Bongo Movie wamemtamani na kumsajili? Haji sasa ni staa wa Bongo Movie na walienda naye Zenji kwenye honeymoon ya Swahiliflix.LEVY: Haji Manara huyu ambaye katenguliwa kwenye eneo lake la kujidai pale Msimbazi? Kama ni huyo mwache aende Bongo Movie. Maana soka la maneno meengi lilishaachwa. Ndo maana Mourinho na Jamhuri Kihwelo wametoweka kama jina la Jack Pemba kwenye muziki wa dansi.


LUQMAN: Haji Manara staa wewe, uliona alivyong’arisha Simba Day? Haji bado yupo sana Simba.


LEVY: Kwani hata Komandoo Hamis Kilomoni si bado yupo Simba? Hata yule bwege shetani bado yupo duniani ila hana mamlaka.


LUQMAN: Shetani unamwita bwege huogopi? Sasa mbona kwenye matendo kadha wa kadha huwa unafuata nyayo zake?


LEVY: Unaweza kufuata nyayo za mtu ili umuue. Kama nafuatilia nyayo zake ujue nataka kumuua. Ila spidi yako ya kufuatilia nyayo zangu za kumfuatilia shetani ni kubwa sana. Unataka kunipiku?


LUQMAN: Mungu na shetani kila mmoja angekuwa na akaunti Insta. Unajua shetani angekuwa hana followers, ila akaunti yake ingekuwa inatembelewa kuliko Mungu.


LEVY: Kwanza shetani akaunti yake ingekuwa ‘praiveti’ na angekuwa anapost usiku tu na bado angekuwa na wafuasi wengi zaidi. Mpaka sasa shetani ana wafuasi wengi duniani. Hata ukiangalia kwenye soka, timu yenye lundo la mashabiki duniani ni Mashetani Wekundu.


LUQMAN: Kwa mujibu wa Instagram, Haji Manara anakubalika Simba kuliko MO Dewji. Haji ana wafuasi Milioni 1.4, MO milioni 1.1. Ipe caption hiyo picha.


LEVY: Ana wafuasi wengi asiowalipa hata posho. Wabongo wanapenda majungu, kusengenya na fitina. Na ndo mchongo unaomng’arisha Manara pale Msimbazi.


LUQMAN: Kwani umewahi kumwonea wivu Haji?


LEVY: Alipokuwa Zenji na Bongo Movie au?


LUQMAN: Najua basi? Nimeuliza tu! Hivi inashindikana Bongo tukawa na sekta ya viwanda vya majungu, fitina, uchonganishi na kujikombakomba?


LEVY: Na ndo jukumu pekee tunalolitenda kwa ubora wa hali ya juu..Haya mengine tunapoteza muda tu. Kungekuwa na mashindano tungekuwa mabingwa wa dunia miaka 58 mfululizo.


LUQMAN: Soudy Brown wa Shilawadu ana followers milioni 3.3 Instagram, MO Dewji wa mwenye viwanda vyake ana milioni 1.1. Bakhresa hana hata akaunti. Ipe caption hiyo picha katika zama hizi za Tanzania ya Viwanda.



LEVY: Ndo ujue MO anataka kuishi Kibongo Movie au Kibongo Fleva sana. Marafiki zake wenyewe ni kina FA, Flaviana Matata, Steve Nyerere, Hamisa Mobetto. Hivi Vanessa Mdee ni rafiki yake pia au ‘rolu modo’ wake?


LUQMAN: Kuna ubaya gani kuwa na marafiki mastaa? Trump mshikaji wake Kanye West. Obama wanaye ni Jay Z, Beyonce, P Piddy na wengine. Bill Clinton enzi zake ungemkuta kaminya na ‘chizi fresh’ wa kikapu, Dennis Rodman. MO anakuumiza nini?


LEVY: Wewe ndo unaumizwa na followers wa Manara. Unatamani wingi wa pesa za MO zigeuke followers ili awe nao bilioni elfu moja na ushee au?


LUQMAN: Toronto Raptors ndio mabingwa wa NBA 2018-2019. Jamaa wa Canada wamevunja dari ya kioo na kuumaliza ubabe wa GS Warriors. Unajua kama Rais wa Toronto Raptors, Masai Ujiri yupo hapa Bongo?


LEVY: Washitue dada zako wa Bongo Movie. Waambie waachane na wanasiasa wa SADC hawana hela wamekuja kupiga blabla tu. Hilo Don la Toronto Raptors ndo danga la uhakika.


LUQMAN: Wanamjua basi? Jamaa ana wafuasi 3,500 Instagram. Wao ili wamjue mtu lazima aonekane sana Insta.


LEVY: Bongo Movie wanampenda mtu ambaye ana shobo mkukuta. Ana pesa za ghafla. Ana matumizi mkurabita. Ana shinda baa. Ana madem wengi. Yaani hakuna kitu wanapenda kama kushindania danga. Ukiwa na madem wengi wengi basi utahusudiwa na Bongo Movie.


LUQMAN: Umeongea lugha ya Wababeli. Umeusimamisha ukweli kwenye kilele cha mnara wa ulinzi. Umeisema iliyo haki. Pokea ukarimu wa Muumba ewe mtumishi Dokta Levy.


LEVY: Ameen. Naomba kuuliza hivi mdhamini wa Ligi Kuu Bongo amepatikana? Na mdhamininwa Miss Tanzania? Kama utaweza nijibu hata suala la Wasafi Festival na Fiesta mwaka huu pia itafanyika? Na mazishi ya Kill Music Awards yalishafanyika au bado maiti ipo mochwari? Pia itafaa unijibu na maendeleo ya Rich Mavoko nje ya WCB. Na kama itakupendeza nijulishe na SwahiliFlix na Steve Nyerere na Uwoya wake wamefikia ‘epsodi’ ya ngapi kwenye tantalila zao? Usiache kunipa na tathimini ya Aslay.


LUQMAN: Unauliza maswali mengi, sasa sijui ujibiwe lipi? Ngoja tunaojua kuuliza maswali tuulize; Hivi kati ya Shiboub wa Simba na Molinga wa Yanga nani mchezaji wa kulipwa?


LEVY: Kuna mchezaji asiyelipwa? Kina Yondani, Dante na Juma Abdul wenyewe walipokosa malipo yao walisusa kambi ya matikiti. Unauliza maswali ya soka bila ‘skillzi’. Ngoja wenye maujanja tukuulize hivi unamuachaje Niyonzima na kumsajili Ajibu? Ndo maana Man U walibadilishana bure Mikhitaryan na Sachez. Kwa sababu walijua majukumu yao yanafanana. Sasa Ajib anafanya alichokuwa anafanya Niyo. Lakini unashindwa kumuongeza mkataba Niyo unatumia mamilioni kwa Ajib ili akakae benchi.


LUQMAN: Hivi Molinga Yanga ndio amesajiliwa baada ya Makambo au sio?


LEVY: Papa Zahera naona anavyowabagaza watani wako. Najiuliza hivi Zahera kasajili wachezaji au kasajili wa laini za chuo? Pale ndugu zetu wameuziwa matikiti pori. Siyo ya Matombo wala Kigwa. Yale ni ya Katavi au Kibondo.


LUQMAN: Kweli aisee, kuna usajili wa laini za simu, usajili wa lini za chuo na usajili wa Molinga Yanga. Wote ni usajili.


LEVY: Hata usajili wa vitambulisho vya taifa. Usajili wa alama za vidole na usajili wa wasanii pale Basata na usajili wa Bolingo sijui Moringe sijui Molinga wa Yanga vyote sawa. Zahera pale amelundika wanaojaribu kuchezea kazi ya kucheza mpira.

Post a Comment

0 Comments