Bigirimana ni tofauti kwa kuwa winga huyo tayari amefuatilia ligi hiyo na amejua namna ambavyo anatakiwa kucheza ili kwenda na kasi ya mashindanoDar es Salaam. Klabu ya Yanga imefanya usajili kabambe kuhakikisha inakuwa na kikosi bora kwa michuano ya msimu ujao.
Usajili huo ni mapendekezo ya Kocha Mwinyi Zahera, ambaye alitaka kuongezwa wachezaji katika sehemu chache ili kuongeza ufanisi.
Yanga imenasa saini za Metacha Mnata, Farouk Shikalo, Ally Ally, Muharami Issa, Lamine Moro, Patrick Sibomana, Maybin Kalengo, Issa Bigirimana na David Molinga.
Miongoni mwa usajili uliotikisa na kitendo cha Yanga kumsajili Bigirimana akitokea APR ya Rwanda.
Winga huyo hakutua Yanga kwa bahati kwani anaifahamu vyema klabu hii tangu akiwa Rwanda.
Katika kuthibitisha hilo, Bigirimana anasema anamfahamu vyema Ibrahim Ajibu akidai ni mmoja wa wachezaji wanaomvutia.Winga huyo anasema Ajibu ni mchezaji hodari aliyekuwa akimfuatilia muda mrefu, lakini atamkosa kwa kuwa nahodha huyo wa zamani wa timu hiyo amerejea Simba.
Akizungumzia usajili wake, Bigirimana anasema alipigiwa simu na mmoja wa viongozi wa Yanga wakitaka huduma yake.
“Kabla ligi haijamalizika nilipigiwa simu nikaulizwa kama nipo tayari kuja Tanzania, mpira ni kazi yangu kwahiyo nikaanza kuisoma Yanga kwa kuangalia sana mechi zao za mwisho nikaona ni timu nzuri,”anasema Bigirimana.
“Yanga si ni timu ndogo kwamba ukiletewa ofa utakataa hii ni timu kubwa na kila mchezaji anataka kuitumikia,” anasema winga huyo.
Ligi Kuu
Baadhi ya wachezaji wa kigeni wanapokuja nchini wanashindwa kuzoea mazingira mapema na aina ya soka ambalo linachezwa.
Kwa upande wa Bigirimana ni tofauti kwa kuwa winga huyo tayari amefuatilia ligi hiyo na amejua namna ambavyo anatakiwa kucheza ili kwenda na kasi ya mashindano.
“Nimeangalia ligi kupitia Azam ingawa ni mechi chache, lakini nimeona nahitaji kutumia nguvu nyingi ili nicheze,” anasema Bigirimana.
Kambi
Yanga katika kuonyesha haitanii kwani muda mfupi baada ya Bigirimana kufika nchini moja kwa moja alipelekwa mkoani Morogoro.
Kambi ya Morogoro ikiwa chini ya kocha msaidizi Noel Mwandila kabla ya Zahera kuwasili.
Bigirimana anasema mazoezi waliyopata kambini yatawasaidia katika ushindani wa Ligi Kuu msimu ujao.
“Mazoezi ni mazuri kwa kweli unapewa zoezi ambalo unaoa linaingia katika mwili mpaka ukitoka uwanjani unakuwa hauna kazi nyingine zaidi ya kupumzika.
“Naamini pamoja na mbinu ambazo tunapewa lazima tutaleta ushindani katika ligi msimu ujao,” anasema Bigirimana.
Ushindani
Si kila mchezaji ambaye anatoka nje anapata nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza, hilo Bigirimana pia anatambua.
Suala hilo limeanza kumuweka na mawazo winga Birigimana ambaye ameanza kupiga hesabu za namba katika kikosi msimu ujao.
“Namba ni changamoto kwasababu wachezaji wote wanajituma mazoezini, ukiangalia unaona kuna ugumu lakini hilo inabidi tupambane zaidi,” anasema.
Ajibu/Simba
Bigirimana anasema anaifahamu Simba ni klabu kubwa ambayo imekuwa na ushindani katika soka ya Afrika.
Winga huyo hakusita kumtaja kinara wake wa mabao Meddie Kagere kuwa ni mchezaji mwenye kiwango bora cha kuvuta katika soka ya Afrika Mashariki na Kati.
Kagere ni mchezaji wa timu ya Taifa ya Rwanda ‘Amavubi’ na msimu uliopita alitwaa tuzo ya mfungaji bora baada ya kufunga mabao 23.
Mbali na Kagere, Bigirimana anamtaja Ajibu ni mchezaji wa aina yake katika soka ya Tanzania.
“Kuna kijana mmoja alikuwa akivaa jezi namba 10 Yanga (Ibrahim Ajibu) ni mchezaji mzuri, lakini kwa kuwa amejiunga na Simba hakuna tatizo tutakabiliana naye,” anasema Bigirimana.
A
0 Comments