Windows

Aussems aibua jambo Simba



KOCHA Mkuu wa Simba, Patrick Aussems, amefurahi na kusema wachezaji wake walicheza kama watoto, licha ya ushindi wa mabao 3-1 ilioupata timu yake dhidi ya JKT Tanzania juzi Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Simba ilipata ushindi huo katika mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Akizungumza baada ya kumalizika kwa mchezo huo, Aussems alisema anaamini kikosi chake kilistahili kushinda idadi kubwa zaidi ya mabao katika mchezo huo, lakini kutokana na umakini mdogo wa wachezaji wake wakapata matokeo waliyopata.

“Tumepata ushindi wa mabao 3-1, matokeo ambayo sijaridhishwa nayo kutokana na aina ya wachezaji nilioa nao kikosini, tulitakiwa kufunga mabao manne hadi sita lakini makosa ya kitoto waliyofanya yamesababisha tupate tulichopata,” alisema.

Alipoulizwa sababu ya kuwatumia wachezaji ambao baadhi wamekuwa wakianzia benchi alijibu kuwa alifanya hivyo kutokana na wengine kusumbuliwa na majeraha.

Aussems alisema wanaanza upya na kuachana na matokeo ya nyuma baada ya timu yake kutupwa nje ya Ligi ya Mabingwa Afrika ikiwa hatua ya awali na timu ya UD Songo ya Msumbiji.

Wekundu hao walifungashiwa virago, baada ya kulazimisha suluhu ugenini jijini Beira, kisha kutoka sare ya bao 1-1 , Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Matokeo hayo yaliifanya UD Songo isonge mbele kwa faida ya bao la ugenini.

Aussems alisema amewatengeneza wachezaji wake kisaikolojia ili wasahau yaliyopita na kuwekeza akili zao kuhakikisha wanapata matokeo mazuri Ligi Kuu na kutetea ubingwa wao.

“Tulihuzunika kwani haikuwa rahisi kupokea matokeo yale, lakini kwenye mpira lolote linaweza kutokea, hata hivyo tumesahau yaliyopita na sasa macho na nguvu zetu zote tumehamishia Ligi Kuu,” alisema.

Simba inashika nafasi ya pili wa Ligi Kuu, ikiwa na pointi tatu, sawa na Lipuli, Azam, Kagera Sugar, Namungo, Mwadui, Polisi Tanzania na Ruvu Shooting, zikitofautiana kwa wastani wa mabao ya kufunga na kufungwa.

Post a Comment

0 Comments