Windows

Taifa Stars yatolewa AFCON 2019, yashindwa kuvunja rekodi ya mwaka 1980


Tanzania imekamilisha ushiriki wake wa Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2019 kwa kuchapwa mabao 3-0 usiku wa Jumatatu katika mchezo wa mwisho wa Kundi C Uwanja wa Al Salam mjini Cairo nchini Misri.

Kipigo hicho kinamaanisha Taifa Stars inaondoka Misri bila hata pointi moja, ikishika mkia kwenye kundi hilo, nyuma ya jirani zao, Kenya waliovuna pointi tatu, ingawa nao pia wanarejea nyumbani, huku Senegal iliyomaliza na pointi sita katika nafasi ya pili ikiungana na Algeria iliyokusanya pointi tisa kwenda hatua ya 16 Bora.

Taifa Stars ya kocha Emmanuel Amunike imeshindwa kuvunja rekodi ya kikosi cha mwaka 1980 kilichoshiriki fainali hizo mjini Lagos, Nigeria ambacho angalau kiliambulia pointi moja baada ya sare na Ivory Coast ya 1-1, kikitoka kufungwa 2-1 na Misri na 3-1 na wenyeji, Nigeria.

Katika mchezo wa jana, mabao yaliyoizamisha Taifa Stars yalifungwa na mshambuliaji wa FenerbahceI ya Uturuki, Islam Slimani dakika ya 34 na kiungo wa Napoli ya Italia, Adam Ounas dakika ya 39 na 45 na ushei.

Ikumbukwe mechi mbili za mwanzo, Taifa Stars ilichapwa mabao 2-0 na Senegal na 3-2 na Kenya ikishiriki fainali za AFCON kwa mara ya kwanza baada ya miaka 39.


Post a Comment

0 Comments