Jengo la Tatu la Abiria (Terminal III) la Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam, litazinduliwa rasmi Agosti mosi na Rais John Magufuli.
Katika hatua nyingine, Waziri Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe amesema Rais Magufuli ameagiza kununuliwa kwa ndege nyingine tatu.
Aliyasema hayo wakati wa utiaji saini wa mradi wa ujenzi wa daraja la Kigogo - Busisi na kudai kuwa wanasiasa wamekuwa wasumbufu kwa kuwa wanatumia hila kujipatia fedha kutoka kwa wakandarasi kwa kigezo cha kuwasaidia kupata zabuni. Waziri Kamwelwe alisema Rais Magufuli atazindua rasmi uwanja huo, baada ya Serikali ya Awamu ya Tano kukamilisha ujenzi wake pamoja na kuwepo kwa mipango ya wafadhili kutaka kukwamisha.
"Historia ya ule uwanja Mfugale (Patrick- Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Taifa wa Barabara) anaijua, ni kweli tuliingia mikataba na wafadhili kuwa watatupa fedha, lakini hawakutupa, tumelipa mpaka tumemaliza kwa fedha za ndani"; alisema.
Alisema baada ya kuanza kwa ujenzi wafadhili hao walijitokeza na kutaka kutoa fedha lakini baada ya wataalamu kuchunguza kwa makini mikataba hiyo ilibainika kuwa kulikuwa na mtego wa kupanga Tanzania kulipa fedha nyingi endapo isingelipa deni kwa wakati.
"Wafadhili walikuwa wameweka mtego kuwa Tanzania ikishindwa kulipa mkopo wa ujenzi kwa wakati waendelee kudai riba kwa ucheleweshaji.
"Walitutega ili tukishindwa kulipa waendelee kutuletea madai ya kuwa tumechelewa kulipa hivyo watudai na riba, lakini bahati nzuri tukashitukia," alisema Waziri huyo.
Alisema "Kuna taasisi za Ulaya zinasema zina fedha za kutukopesha, hatukatai lakini ziwe na masharti nafuu hawawezi kusema tunawapa hela tunaleta na mkandarasi."
Ushawishi wa wanasiasa Kamwelwe aliwashukia wanasiasa na kuwataka kuacha mara moja tabia ya kuingilia kazi za kitaalamu badala yake waache wenye taaluma husika wafanye kazi. "Hizi kazi ni ngumu kidogo, ujenzi wa bwawa la kufua umeme liliingiliwa na mamluki, alipewa Mtanzania kutengeneza taarifa ya mazingira akasema wananchi wakienda kuishi kule watachafua mazingira, hadi Rais (John Magufuli) aliingilia akasema yeye atafanya.
0 Comments