Naibu Waziri wa Afya Dkt. Faustine Ndugulile amekamilisha ziara yake Mkoani Kigoma baada ya kutembelea Mpaka wa Manyovu ili kujionea hali ya utayari wa Mkoa huo katika kukabiliana na ugonjwa wa Ebola.
Pia ametembelea ujenzi wa Hospitali mpya ya Wilaya ya Buhigwe ambayo itakua ni tegemeo kwa wananchi wa eneo hilo baada ya kukosa huduma za afya huku wakilazimika kutembea umbali mrefu kwenda Hospitali ya Heri Mission inayomilikiwa na taasisi ya kidini. Dkt. Ndugulile amemtaka Mkuu wa wilaya hiyo Kanali Mikael Ngayalina kuhakikisha anasimamia ujenzi huo ili ukamilike kwa wakati na kuanza kutoa huduma mapema iwezekanavyo.
Pamoja na hayo, ametembelea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kigoma ya Maweni ili kuona hali ya utoaji huduma Hospitalini hapo huku akitoa ahadi ya Serikali kupeleka mashine 5 za dialysis kwa ajili ya kusafisha damu kwa wagonjwa wa figo, pia ameahidi kutatua changamoto ya uhaba wa watumishi kwa kupeleka watumishi wapya watakaoajiriwa mwaka ujao wa Serikali.
Vile vile amesema Serikali itapeleka fedha kwaajili ya kusaidia ujenzi wa OPD mpya ya kisasa, Emergency na ICU ambapo majengo hayo hayapo hivi sasa.
0 Comments