Windows

Katibu Mkuu Jumuiya ya Madola afanya mazungumzo na Prof. Kabudi


Jumuiya ya Madola imeonesha kuridhishwa na namna Tanzania inavyotekeleza mageuzi ya kiuchumi, uwajibikaji na utawala bora kwa wananchi wake jambo ambalo jumuiya hiyo inalihimiza na kulisimamia kwa nchi wanachama wake.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola Bi Patricia Scotland wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi katika ofisi za sekretarieti ya jumuiya hiyo zilizopo London Nchini Uingereza.

Katika mazungumzo hayo Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola Bi Patricia Scotland ameeleza kuridhishwa na maelezo yaliyotolewa na Profesa Kabudi kuhusu utekelezaji wa masuala ya demokrasia,utawala bora na utawala wa sheria pamoja na Haki za binadamu nchini Tanzania na kwamba Jumuiya hiyo inatambua  juhudi hizo na inaunga mkono hatua hiyo.

Katibu Mkuu huyo ameongeza kuwa mbali na kuhimiza utekelezaji wa utawala bora, haki za binadamu na utawala wa sheria pia Jumuiya ya Madola imelenga kukuza na kuwezesha biashara miongoni mwa nchi wanachama ikiwa ni pamoja na fursa zilizopo kupitia shirika la biashara la kimataifa (WTO) na mashirikiano ya biashara ya kikanda.

Amesema ni jukumu la nchi za Jumuiya ya Madola kuhakikisha uwepo wa amani na utulivu katika jumuiya hiyo ili kuiwezesha kupiga hatua za haraka za kimaendeleo na kuifanya  Jumuiya nzima kuendelea bila ya kuacha nchi nyingine nyuma kutokana na uwepo wa migogoro ama machafuko ya wenyewe kwa wenyewe miongoni mwa wanachama wa Jumuiya. Katika hili ameisifia Tanzania kwa kuwa na Amani na utulivu muda wote na pia kushiriki katika juhudi za kutatua migogoro kwa nchi zingine wanachama na wasio wanachama wa Jumuiya.

Kuhusu suala la mabadiliko ya tabia nchi,Katibu Mkuu huyo wa jumuia ya madola amesisitiza umuhimu wa ushirikiano miongoni mwa nchi wanachama wa Jumuiya hiyo ili kukabiliana na athari zitokanazo na mabadiliko ya tabia nchi. Ameeleza kuwa Jumuiya hiyo itaendelea kushirikiana na Tanzania katika program mbalimbali zinazolenga kukabiliana na madhara ya mabadiliko ya tabia nchi na masuala ya mazingira kwa ujumla.

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. palamagamba John Kabudi amemhakikishia Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola kuwa Tanzania inaipa umuhimu mkubwa jumuiya hiyo na itaendelea kushirikiana nayo katika masuala ya ukuzaji wa uchumi, utawala bora hususani wakati huu ambapo Tanzania inafanya mageuzi ya kiuchumi katika kuelekea kuwa nchi ya uchumi wa kati.

Post a Comment

0 Comments