Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa anatarajia kukutana na wafanyabiashara wote nchini kupitia utaratibu uliohusisha uundwaji wa kanda za mikoa yenye lengo la kutafuta ufumbuzi wa kero mbalimbali zilizojitokeza katika mkutano wa wafanyabiashara hao na Rais John Magufuli Juni, mwaka huu.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Bashungwa alisema pamoja na mambo mengine ziara hiyo itakayofanyika katika kanda saba alizoziunda zitahusisha Kanda za Kusini, Kaskazini,Mashakariki, Magharibi, Kanda ya Kati, Nyanda za Juu Kusini na Kanda ya Pwani.
Alisema utaratibu huo maalumu utakaoanza hivi karibuni, umelenga kuwafikia wafanyabiashara wote wakiwemo wenye viwanda, ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais Magufuli aliyeitaka wizara hiyo kufika maeneo ya viwanda yaliyopo nchini nzima na kushughulikia kero wanazokabiliana nazo.
"Katika mkutano wake na wafanyabiashara uliofanyika Juni 07 mwaka huu pale Ikulu, Rais alitusaidia kwa kubainisha changamoto mbalimbali zilizojitokeza na kututaka tuzitatue, hivyo nami katika kulitekeleza hilo nimekutana na timu yangu na kuamua kuunda kanda hizo kwa lengo la kwenda kusikiliza kero zao na kuzitatua,"alisema Bashungwa.
Alisema hatua hiyo inayotekelezwa na Serikali, zaidi imelenga kuweka mazingira wezeshi kwa wananchi ya kufanya biashara na ujenzi wa viwanda unaoendana na mpango wa uchumi wa kati wa viwanda ifikapo 2025 ambao kwa sasa utekelezaji wake unakwenda kwa kasi.
Aliitaja mikoa itakayohusika katika kanda hizo kwa kuanza na kanda ya kati kuwa ni Dodoma, Singida na Tabora huku kwa upande wa kanda ya kusini ziara hiyo itahusisha mikoa ya Ruvuma, Lindi na Mtwara.
Aidha alisema kanda ya kaskazini itahusisha mikoa ya Manyara, Arusha, Tanga na Kilimanjaro huku Kanda ya Mashariki ikihusisha mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Morogoro; pia kanda ya nyanda za juu kusini ambapo ziara hiyo itaihusisha mikoa ya Mbeya, Iringa, Njombe pamoja na Songwe.
Waziri Bashungwa aliitaja mikoa atakayofanya ziara hiyo ya kukutana na wafanyabiashara hao kwa upande wa kanda ya Magharibi kuwa ni Rukwa, Katavi pamoja na Kigoma huku ziara katika kanda ya Ziwa ikiihusisha mikoa ya Kagera, Mara, Geita, Simiyu pamoja na Mwanza.
0 Comments