Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imeibuka mshindi wa kwanza kwa utoaji wa huduma za afya na matumizi ya Teknolojia katika tiba kwenye maonesho ya 43 ya Kibiashara ya kimataifa ya Dar es Salaam.
Kombe hilo la ushindi ilitolewa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan wakati akifungua maonesho hayo yanayofanyika katika uwanja wa Julius Kambarage Nyerere uliopo barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam.
Tangu kuanza kwa maonyesho hayo tarehe 28/06/2019 katika banda la Taasisi hiyo jumla ya wananchi 660 wamefanyiwa vipimo vya magonjwa ya moyo ambapo asilimia 60 wamegundulika kuwa na uzito mkubwa asilimia 40 shinikizo la juu la damu na asilimia 4 wana kiwango kikubwa cha sukari katika damu (hyperglycemia).
Akizungumza na Mwandishi wa habari hizo Maria Samlongo ambaye ni Afisa Lishe wa Taasisi hiyo alisema wananchi wengi hawapati mlo ulio kamili na wenye virutubisho vya kutosha hivyo basi wameona watoe elimu ya lishe ili wananchi wafahamu jinsi ya kuandaa chakula bora katika jamii zao.
Maria alisema baada ya kufanyiwa vipimo watu wengi walionekana uwiano wao wa urefu na uzito haulingani hivyo kupelekea wengi wao kuwa na uzito mkubwa zaidi.
“Watu wengi nilioonana nao wanaamini viywaji vyenye sukari kama soda, juisi na pombe haviongezi uzito kitu ambacho siyo kweli nimewashauri kuachana na vinywaji hivyo na kupendelea zaidi kutumia matunda kama yalivyo ,” alisema Maria.
Mtaalamu huyo wa lishe aliendelea kusema kuna baadhi ya watu wanaamini wakiacha kula mlo wa asubuhi na mchana watapungua uzito kitu ambacho siyo sahihi kwasababu ikifika jioni wanashikwa na njaa kali na kuwafanya kula kiasi kikubwa cha chakula kuliko uhitaji wakati wa usiku hali inayowapelekea ongezeko kubwa la uzito.
Wanachotakiwa kufanya ni kugawa milo yao vizuri kuanzia asubuhi hadi jioni kitu cha kuzingatia ni mlo wa jioni kuwa mwepesi hasa kula mboga za majani, matunda na vyakula vya protini kidogo.
Kwa upande wake Gasper Minja aliyefika katika banda hilo kwa ajili ya kupima afya aliishukuru Taasisi hiyo kwa kutoa huduma za ushauri na upimaji wa magonjwa ya moyo bila malipo yoyote.
0 Comments