Windows

Hizi ndio sababu za upungufu wa nguvu za kiume, Wanaume kupewa dawa


Imeelezwa kuwa asilimia 85 ya upungufu wa nguvu za kiume kwa wanaume unatokana na magonjwa ya moyo na kisukari, hivyo Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) imeamua kuleta dawa za kurejesha nguvu hizo wakati wanaume wakiendelea na matibabu ya vishawishi.

Dawa hizo zinatolewa katika Viwanja vya Maonesho vya Mwalimu Julius Nyerere vilivyopo Barabara ya Kilwa katika Maonesho ya 43 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam, ambapo taasisi hiyo katika banda lao wanatoa huduma bure ya upimaji, ushauri na dawa.

Akizungumza katika viwanja hivyo, Daktari bingwa na Mkuu wa Idara ya Utafiti na Mafunzo wa taasisi hiyo, Dk Pedro Pallangyo alisema kuwa wanatoa huduma za vipimo bure vya urefu, uzito, mapigo ya moyo, shinikizo la damu, sukari, kipimo cha umeme wa moyo (ECG) na kipimo cha utendaji kazi wa moyo (ECHO).

Alisema pia kuna mtaalamu wa lishe anayetoa ushauri bure wa lishe na ushauri na baada ya vipimo, watakaobainika kuwa na magonjwa ya moyo na magonjwa ambatano ya kifua, ganzi, shinikizo la damu na upungufu wa nguvu za kiume watapatiwa dawa.

"Kwa kiwango kikubwa upungufu wa nguvu za kiume unatokana na magonjwa ya moyo na kisukari huku chakula kikisababisha kwa kiwango kidogo cha asilimia tano, hivyo kwa wenye upungufu wa nguvu tuna dawa zitakazowasaidia kwa saa 24 hadi 48 wakati wakiendelea na matibabu ya chanzo cha ugonjwa,"alisema Dk Pedro.



Post a Comment

0 Comments