


YANGA imezidi kunoga baada ya tukio lao la juzi lililowakutanisha wadau wa klabu hiyo, sambamba na harambee waliyoiendesha kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam, iliyowawezesha kuvuna mamilioni ya fedha zitakazowasaidia katika usajili.
Katika tukio hilo, Mgeni rasmi alikuwa ni Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, aliyewaongoza wageni wengine, akiwamo Rais mstaafu Jakaya Kikwete, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.
Viongozi hao kila mmoja alipokewa kwa aina yake na wadau wa Yanga waliofika ukumbini hapo, lakini utamu zaidi ulikuwa wakati wa kutoa michango.
Kilichochangia shangwe hizo ni kutokana na ahadi zilizotolewa na Wanayanga hata wale ambao hawakuwapo ukumbini walipiga simu na kuahidi kiasi cha fedha wanachotoa.
Licha ya ahadi nyingi kutolewa, zilizopokelewa kwa shangwe kubwa ni ile ya mfanyabiasha maarufu hapa nchini, Rostam Aziz, kapuni ya GSM na Makonda.
Ahadi ya Rostam ilitangazwa na Waziri Mkuu Majaliwa, mfanyabiashara huyo akiahidi kutoa sh milioni 200, lakini inadaiwa baada ya shughuli hiyo, alipiga simu na kuahidi kutoa kiasi kikubwa zaidi ambacho hakupenda kiwekwe wazi.
Kwa upande wa GSM, walitoa sh milioni 300, huku Makonda akiahidi kuwapa Yanga uwanja, Kigamboni, Dar es Salaam, kitendo kilichowafurahisha mno watu wa Yanga, wakisisitiza uamuzi wake huo ni wa kiuanamichezo hasa.
Hata hivyo, BINGWA limepenyezewa taarifa kuwa watu walijitokeza zaidi wengi kuichangia Yanga, wakiwa hawataki kutajwa majina.
Kutokana na michango hiyo, hadi jana inadaiwa Yanga ilikuwa imejikusanyia kati ya sh bilioni 2-4, wakiwa wamevuka lengo la awali la sh bilioni 1.5.
Katika hatua nyingine, utambulisho wa mshambuliaji mpya wa Yanga, Juma Balinya, umewapagawisha mno Waganda ambao walikuwa wakifuatilia tukio hilo la juzi, wakimtabiria kung’ara zaidi Jangwani kuliko hata ilivyokuwa kwa Emmanuel Okwi wa Simba.
Wapenzi wa soka wa Uganda juzi na jana, walikaririwa na vyombo vya habari nchini humo wakisema kuwa Balinya ndiye mfalme mpya wa soka la Tanzania kwa wachezaji wa kigeni.
Walisema kwa mapokezi aliyopata mchezaji huyo na uwezo wake uwanjani, utamfanya kupambana hasa ili kutowaangusha Yanga, huku wakiipongeza klabu hiyo kwa kulamba ‘dume’, kwa mujibu wa mtandao wa futaa.
Wakati huo huo, Kamati ya Utendaji na ya Usajili ya Yanga, imekutana jana na kufanya kikao kizito kujadili mambo mbalimbali kuhusu matumizi ya fedha walizopata, zaidi wakilenga usajili.
Kwa taarifa ambazo BINGWA imezipata kutoka chanzo cha ndani ya Yanga, kamati hizo zimekutana ili kuiruhusu timu ya usajili kwenda Misri kufanya kweli.
Imeelezwa kuwa baadhi ya wajumbe wa kamati ya usajili wakiongozana na Mwenyekiti wao, Frank Kamugisha, walitarajiwa kuondoka usiku wa jana kuelekea Misri kukutana na Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera.
Mtoa taarifa huyo alisema lengo la safari hiyo, ni kwenda kumalizina na wachezaji wanne wanaowahitaji, pia kumpelekea Zahera orodha ya nyota aliotaka wasajiliwe.
“Leo usiku (jana), timu ya usajili inatarajia kuondoka kwenda Mirsi kukutana na kocha Zahera, lakini kuna wachezaji wanne wanakwenda kumalizana nao, wawili wazawa, wawili wa kigeni.
“Majina ya wachezaji hao siwezi kuyataja hadi pale mambo yatakapokamilika, lakini kama kocha atahitaji wachezaji zaidi, ataongezewa ndio sababu ya kukutana naye,” kilisema chanzo hicho.
Mawakala wapigana vikumbo Jangwani
Baada ya kusikia kuwa Jangwani wametenga mkwanja mkubwa kwa ajili ya usajili, unaambiwa mawakala wamekuwa wakipigana vikumbo wakifukuzia nafasi ili wasajiliwe.
Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela, amethibitisha kuwapo kwa hali hiyo na kusema kila siku lazima wapokee simu za mawakala au maombi ya wachezaji wakitaka nafasi katika timu hiyo.
Alisema mawakala hao, wamekuwa wakisumbua kila kukicha, wengine wakienda moja kwa moja klabuni, wengine wakipiga simu au kutuma video za wachezaji wao.
“Suala la mawaka kujitokeza kwa wingi kuleta wachezaji wao ni kweli, kila siku, usipopokea simu, basi utaletewa mchezaji umuone au video yake uangalie, email (anuani peke) ya Yanga imejaa maombi.
“Hali hii haijaanza kipindi hiki, tangu mwishoni mwa msimu, ila kwa sasa wamezidi, lakini tupo makini na kile tunachofanya,” alisema Mwakalebel



0 Comments