Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limebaini udanganyifu mkubwa uliofanywa kwa baadhi ya waombaji wa nafasi za kujiunga na jeshi hilo na limetangaza kufanya mapitio ya usaili.
Limesisitiza kuwa hatua kali zitachukuliwa, kwa wote watakaobainika kufanya udanganyifu huo.
Akizungumza Makao Makuu ya Jeshi, Upanga jijini Dar es Salaam , Mkurugenzi wa Habari, Luteni Kanali Gervas Ilonda amesema jeshi hilo watashirikiana na mamlaka nyingine ikiwemo Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA), Baraza la Vyuo vya Ufundi (NACTE), Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na Jeshi la Polisi katika kufanya operesheni kabambe ili kubaini waliofanya udanganyifu.
Luteni Kanali Ilonda alisema pia watatumia madaktari wao, kurudia kuwapima upya afya vijana hao ambao tayari wameshajiandikisha kwa kile alichoeleza kuwa baadhi yao wamedanganya kuhusu afya zao.
"Watakaobainika kutoa taarifa za uongo watakamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria, na si wao tu hata ambao wamefanikisha vijana hao kufanya udanganyifu nao tutawashtaki.
"Kijana atasema aliandikishwa na ofisa gani, tuna taratibu zetu za jeshi tukiwabaini tutawachukulia hatua, kuna viongozi ambao wameshiriki, kuna watu ambao waliwaongoza hao vijana na kuwaelekeza namna ya kufoji, kuna waliosaidia kufoji, kuna madaktari waliotoa ripoti ya uongozi kuhusu afya, hii cheni yote ijiandae, amesema.
Alisema wapo viongozi wamekuwa wakitumia madaraka yao vibaya, kwa kutaka vijana wao wasajiliwe jeshini.
"Kiongozi unakuta anakuja na vijana 10 mpaka 20 na anakuwa na idadi hiyo kwa mikoa tofauti tofauti. Mfano akipeleka 20 JWTZ, 20 JKT kwa mikoa mitano tayari ni vijana 100 watapewa mafunzo ya kijeshi kumbe ana malengo yake baadaye aje awatumie kwa faida zake, na hapo ndio wanazaliwa vikundi visivyofaa,"alisema.
Luteni Kanali Ilonda alisema pia baadhi ya wazazi na vijana, hupuuza taratibu zilizowekwa na kusisitiza vijana wao wachukuliwe nje ya utaratibu au wachukuliwe hata kama wana upungufu katika sifa zilizotangazwa ikiwemo elimu, umri, afya, na wengine wakidanganya kuwa ni yatima.
"Napenda kuweka bayana vigezo vyote vilivyowekwa kwa ajili ya kupata vijana wa JKT ni muhimu na ni lazima vikamilike, ukiwa una upungufu usipoteze muda kuomba maana hutofanikiwa," alisema Ilonda.
Alitaja vigezo vinavyozingatiwa ni awe raia wa Tanzania, umri, vijana wenye elimu ya darasa la saba umri ni miaka 16 hadi 18, wenye elimu ya kidato cha nne umri usizidi miaka 20, elimu ya kidato cha sita umri usizidi miaka 22, wenye elimu ya Stashahada umri miaka 25 na wenye elimu ya Shahada umri usizidi miaka 26.
Pia wenye Shahada ya Uzamili umri usizidi miaka 30, wenye Shahada ya Uzamivu umri usizidi miaka 35 na kwamba awe na afya njema, akili timamu, na asiwe na michoro mwilini, mwenye nidhamu, na ambaye hajapatikana na hatia mahakamani na hajawahi kufungwa.
Alitaja vigezo vingine watakavyovipitia ni cheti halisi cha kuzaliwa, cheti halisi cha shule na matokeo na cheti halisi cha matokeo, asiwe ametumikia Jeshi la Polisi, Magereza, Chuo cha Mafunzo (KMKM) wala kuajiriwa idara nyingine ya serikali.
0 Comments