Raia watatu wa Jamhuri ya Watu wa China wamekamatwa na Polisi wa Kanda Maalumu ya Tarime/Rorya, wakituhumiwa kwa kupatikana na vifurushi tisa vyenye madini aina mbalimbali, yakiwamo dhahabu, aluminium oxide, silicon oxide, iron oxide, calcium, magnesia na titanium bila ya vibali wala leseni hivyo kuhujumu uchumi.

Wachina hao ni Lin Nchui, Wang Xialong na Wang Zungsong, ambao kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Tarime/ Rorya, Henry Mwaibambe, walikamatwa na askari wa usalama barabarani Juni 12, mwaka huu eneo la Nkende, kilometa mbili kutoka Tarime mjini katika barabara ya Sirari – Musoma.

Kamanda Mwaibambe amesema wageni hao, walikuwa katika gari aina ya Toyota Land Cruiser lenye namba za usajili KBW 515 L, na askari walipopekua ndani ya gari hilo, walikuta kuna vifurushi mifuko tisa ya madini aina mbalimbali na walipohojiwa walidai kuwa hawana vibali wala leseni ya biashara hiyo.

"Tuliwaweka chini ya ulinzi tukiendelea kuwahoji na kuvipeleka vifurushi hivyo vya madini hayo kufanyiwa uchunguzi zaidi kwa wataalamu na maabara ya madini Dodoma na kurejesha majibu kuwa katika mawe hayo kuna madini mbali mbali za sampuli hizo yakiwemo dhahabu, aluminium oxide, silicon oxide, iron oxide, calcium, titanium na magnesia na madini aina nyingi yenye viwango tofauti, amesema Kamanda Mwaibambe.

Alisema baada ya kurejeshwa majibu kutoka Maabara ya Madini Dodoma, wamewafungulia kesi ya kupatikana na madini hayo bila kibali na nyingine ya uhujumu uchumi na utoroshaji wa fedha, na kufikishwa katika Mahakama ya Wilaya Tarime.

Wote watatu walipelekwa mahabusi hadi Julai 5, kesi yao itakapotajwa tena.