Na Amiri kilagalila, Njombe

Shirika lisilo la kiserikali la Njombe youth development organization (NJOYODEO) kwa kushirikiana na umoja wa vijana chama cha mapinduzi (CCM) mkoani Njombe wamewatembelea wafungwa na mahabusu katika gereza la mkoa mpechi  na kutoa msaada  ikiwemo mashuka na mablanketi  ili kuwaondolea dhana ya kwamba kundi hilo limesahaulika katika jamii.


Akizungumza mara baada ya kupokea msaada huo mkuu wa gereza la mkoa wa Njombe SP Charles Myinga amesema idadi kubwa ya wafungwa na mahabusu gerezani hapo wanakabiliwa na kesi za mauaji ambazo chanzo chake ni migogoro ya ardhi, ushirikina na tamaa ya utajiri na kuendelea kuisisitiza serikali na mahakama kuongeza nguvu katika usikilizaji wa kesi za mauaji

Aidha Myinga amesema gereza linakabiliwa na changamoto nyingi hivyo msaada uliotolewa na wadau hao utasaidia kupunguza changamoto licha ya kuwa na uhitaji mkubwa kwa mahabusu,huku jeshi hilo pia likiwa na uhaba wa makazi ya askari.

“Sisi tunatoa shukrani lakini bado uhitaji ni mkubwa na sasa hivi jeshi tunauhaba wa makazi ya askari,na kwa sasa tunafyatua matofari ya kutosha kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za askari kwa hiyo kama kuna wadau wanaoweza kujitolea mabati,misumari,mbao  sisi vyote tunapokea lengo letu askari wapate makazi”alisema Myinga

Hamis Kasapa ni mkurugenzi wa NJOYODEO na Nehemia tweve ni mwenyekiti  wa umoja wa vijana UVCCM mkoa wa Njombe, wamesema  sababu  zilizowagusa kutembelea  katika gereza hilo ni uwepo wa idadi kubwa ya vijana waliofungwa pamoja na mahabusu jambo ambalo linaonyesha kundi la vijana ndiyo nguvu kazi ya taifa lakini idadi kubwa wako hatarini kuishia gerezani .

“Yapo malengo mengi yaliyotufanya kufika hapa kwa  wenzetu waliopo magereza,lakini tumebaini changamoto ambazo wenzetu wanakumbana nazo kuna zingine ni za kawaida ambazo zipo ndani ya uwezo wetu na tunazimuda katika kuzifanyia kazi,lakini kwa changamoto kubwa moja mlundikano wa kesi au kulimbikizwa kwa kesi na muda wa vikao vya mahakama,tutajitahidi kwa nafasi zetu kuona namna gani wanaohusika wanaweza kutusaidiaje ili jambo hili liweze kufanyika kwa wakati,”alisema Nehemia Tweve.

Kwa upande wake Hamisi Hassan Kasapa amesema kuwa  wameahidi  Jully 2 kufikisha screen kwa ajili ya akina baba na akina mama pamoja na radio zitakazoweza kugawanywa spika katika vyumba vya kulala kwa kufuata utaratibu  ili  kuweza kujua nini kinachoendelea katika nchi yao.

Aidha amesema wao kama vijana hawatoi misaada kwa ajili ya kuwadekeza wafungwa isipokuwa ni kufikisha baadhi ya huduma za msingi ambazo wafungwa wanazikosa.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa gerezani  hapo zaidi ya asilimia 70  ya wafungwa wake na mahabusu ni vijana na wana kabiliwa na kesi za za mauaji.