Windows

Tetesi za usajili Simba leo 30 May 2019

UONGOZI wa klabu ya Simba umepanga kuwatoa kwa mkopo nyota wake watatu akiwamo mshambuliaji, Adam Salamba, anayekwenda kukipiga nchini Ureno.
Salamba ambaye alisajiliwa na Simba msimu huu akitokea Lipuli FC kwa dau la Sh milioni 40, amekosa namba ya kudumu katika kikosi hicho cha Msimbazi kinachonolewa na kocha, Patrick Aussems, kutokana na kushindwa kumudu ushindani uliopo.
Uwepo wa washambuliaji hatari kikosini hapo kama vile Meddie Kagere, John Bocco na Emmanuel Okwi, ulikuwa ni sababu tosha kwa Salamba kushindwa kutamba ndani ya Wekundu hao wa Msimbazi.
Chanzo cha uhakika kutoka ndani ya Simba, kimelipasha BINGWA kuwa wachezaji wengine ambao wanatarajiwa kutolewa kwa mkopo baada ya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu kumalizika ni Rashid Mohammed, anayekwenda nchini Kenya na Abdul Mohammed, ambaye haijajulikana atakwenda timu gani.


Aidha, chanzo hicho kilieleza kwamba, tayari Aussems amekabidhi ripoti yake kwa uongozi inayoonyesha wachezaji watakaoachwa lakini hakuwataja kwa majina.
Hata hivyo, mtoa taarifa huyo alisema alichoeleza kocha ni kwamba wataachwa  wachezaji wanne wa kigeni na watatu wazawa.
“Ripoti ya kocha haijawataja kwa majina wachezaji ambao wataachwa msimu huu lakini idadi yao ni saba, ila katika orodha hiyo sidhani kama Zana (Coulibally) atakosekana,” kilisema chanzo hicho.
Katika hatua nyingine, chanzo hicho kilieleza kwamba kiungo mshambuliaji wa timu hiyo, Mohammed Ibrahim ‘Mo’, pia anajadiliwa ili kujiridhisha kama anaweza kubaki kikosini msimu ujao.
“Kimsingi kikosi cha Simba hakitabadilika sana maana tayari tumemwongezea Bocco mkataba, kuhusu wachezaji wapya bado tunazungumza nao ila siwezi kuwaweka wazi,” kilieleza chanzo hicho.

Post a Comment

0 Comments