Na John Walter- Babati

Mkuu wa mkoa wa manyara Alexander Mnyeti ameitaka halmashauri ya mji wa Babati kuzungushia uzio uwanja wa michezo wa kwaraa ili waweze kuingiza mapato kupitia mechi mbalimbali ambazo zitachezwa katika uwanja huo.

Amewapa mbinu hiyo mara baada ya kuona Halmashauri hiyo ikizidi kudidimia kimapato kutokana na kukosa ubunifu wa Miradi itakayowawezesha kuingiza mapato akitolea mfano halmashauri ya wilaya ya Ruangwa yenye timu ya  Namungo Fc na Kinondoni na timu yake ya  Kmc ambao wamefanikiwa kujenga uwanja ambao umewasaidia kuwaingizia mapato mengi kupitia Michezo.

Amesema  kuwa halmashauri hiyo mapato yake yamekuwa yakisuasua  kutokana na kushindwa kubuni vyanzo vipya vya mapato  hali inayosababisha kuishushia hadhi halmashauri hiyo ambayo ina vyanzo vingi vya mapato ambavyo vingeweza kuingiza pesa zaidi ya bilioni 1.2 wanayokusanya kwa mwaka ikiwa pesa hiyo inakusanywa na mfanyabiashara mmoja kwa mwezi.

“Kaeni Mjitafakari upya muone ni jinsi gani mnaweza kwenda mbele zaidi ikiwa ni pamoja na kubuni njia mpya za mapato”alisema Mnyeti

Mkuu wa Mkoa wa Manyara amefanikiwa kutengeneza uwanja wake wilayani Misungwi mkoani Mwanza alipozaliwa unaotumiwa na timu ya Gwambina Fc akisema kuwa ilikuwa ni ndoto yake tangu utotoni.