Na John Walter-Dareda-Babati
Licha ya kucheza bila viatu,Wanafunzi wa chuo cha Uuguzi Dareda wamewalaza wakubwa wao Manyara Athletics Club kwa Mabao 2-1 huku wakijisifu kuwa ushindi kwao ni kawaida.
Kocha wa DaredaNursing,Leonce Maganga anasema michezo katika chuo hicho wameipa Kipa umbele ndio siri ya kushinda michezo yao kila wanapokutana na timu pinzani.
Maganga amesema wiki iliyopita walicheza na wataalamu wa Maabara kutoka Bashnet na kufanikiwa kuwafunga na kwamba huwa hawabahatishi.
Wachezaji wengi wa Dareda walionekana wakisakata Kabumbu bila kuwa na viatu huku mwamuzi akiwaruhusu akijua kabisa sheria za soka haziruhusu mchezaji kucheza peku.
Mwenyekiti wa Manyara Atletics Club Dr. Edward Magoma amesema lengo la Michezo ya kirafiki wanayoendelea nayo kwa sasa ni kujenga uhusuano mzuri na jamii na kujenga afya.
Kwa upande wa Katibu wa Manyara Athletics Dr. Abubakar Mjaka, ameshangazwa na timu hiyo ya wanafunzi wa Nursing Dareda kucheza bila viatu [peku] akiwasisitza kucheza mpira kwa kujituma wakitambua kuwa mbali na ajira lakini pia michezo inajenga afya.
“Ila mmetusikitisha sana wanafunzi ,wengi mmecheza bila viatu hatujajua tatizo ni nini,mjue kuwa leo mmecheza hapa katika uwanja wenu huu lakini mtaenda kwa wengine hamtaruhusiwa kucheza hivyo,mkija kwetu hatutawaruhusu”alisema Mjaka.
Mjaka amesema awali walijua kuwa huo ndio utamaduni wao hivyo wakaamua wasubiri hadi mpira umalizike,huku akiwashauri kuwa wacheze mpira kwa kujikinga .
Hata hivyo hawajaridhika na matokeo hayo na kuahidi kuwaita mjini Babati kwa ajili ya kurudiana nao tena siku za hivi karibuni kujipima nao kwa mara nyingine.
Katika jitihada za kujikinga na maradhi mbalimbali,Madakatari wa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Manyara wameanzisha timu ya mpira wa Miguu ijulikanayo kama Manyara Athletics Club kwa lengo la kufanya mazoezi na kujenga mahusiano mazuri na jamii kwa kucheza michezo ya kirafiki kila baada ya wiki mbili.
0 Comments