NAHODHA wa timu ya taifa na mchezaji wa klabu ya KRC Genk ya Ubelgiji, Mbwana Samatta, leo amepewa tuzo na Global Group kwa kuthamini mchango wake kwenye jamii na kuwa mfano wa kuigwa kwenye sekta ya michezo nchini.
Samatta ambaye ana tuzo ya mfungaji bora kwenye kikosi chake Genk, amefunga mabao 23 na amekabidhiwa tuzo za heshima mbili ambazo ni pamoja na kiatu kilichopewa jina la Mguu wa Dhahabu.
Mhariri Mtendaji wa Group Publishers, Saleh Ally, amesema kuwa sababu kubwa za kutoa tuzo hizo ni kuthamini mchango wa mwanasoka huyo kupitia mafanikio yake licha ya changamoto nyingi zilizopo.
“Tuzo hii ya Kiatu cha Dhahabu 2019 Mbwana Samatta, tumempa kwa sababu amekuwa mfungaji bora katika klabu zote alizopitia, kuanzia TP Mazembe kule DR Congo na sasa katika klabu ya KRC Genk ameonyesha kwamba inawezekana na ni jambo kubwa amelifanya.
“Tuzo hii nyingine ni ya Mfano wa Kuigwa 2019 Mbwana Samatta kwa kuwa ameonyesha mafanikio makubwa katika klabu alizopita kuanzia DR Congo lakini amekuwa mchezaji wa kwanza kutoka Tanzania kucheza mashindano ya dunia ngazi ya klabu akiwa na Thomas Ulimwengu wakati wanacheza TP Mazembe.
Amekuwa mchezaji bora wa Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani, hivyo yote ni mafanikio yaliyotokana juhudi kubwa alizofanya,” alisema Saleh.
Baada ya kupewa tuzo hio, Samatta amesema kuwa anaishukuru kampuni ya Global Group kwa kujali na kumpa heshima hiyo kwani hakutarajia kitu kama hicho.
“Sikutarajia na wala haikuwa kwenye akili zangu kwamba nitapewa tuzo hizo kubwa na za heshima, sina cha kusema zaidi ya kushukuru,” amesema.
PICHA NA RICHARD BUKOS | GPL
The post Mbwana Samatta Apewa Tuzo na Global Group appeared first on Global Publishers.
0 Comments