Katika kuhakikisha timu zote za Yanga zinakuwa imara, uongozi wa timu hiyo umemtangaza Mwinyi Zahera kuwa msimamizi Mkuu wa timu zote
Akizungumza kwenye hafla ya Iftar Gala Dinner iliyofanyika Hotel ya Serena jijini Dar es salaam usiku wa kuamkia leo, Mwenyekiti wa Yanga Dk Mshindo Msolla amesema Zahera ambaye ni kocha wa kikosi cha kwanza, pia atasimamia timu ya Vijana (Yanga B) na timu ya Wanawake (Yanga Princess)
"Kwa sababu ya masuala ya ufundi, natangaza mbele yenu, timu zote zitakuwa chini ya kocha Mwinyi Zahera," alisema Dk Msolla
"Ni lazima kama timu tuwe na filosofia moja. Hivyo tumeona filosofia inayotumiwa kwenye kikosi cha kwanza ni lazima ikafuatwa na makundi yote. Zahera atakuwa msimamizi Mkuu"
ASISITIZA KUVUNJWA MAKUNDI
Dk Msolla amewataka Wanayanga kudumisha umoja ili kuweza kufikia malengo waliyojiwekea
Aidha amesema ahadi walizotoa wakati wa kampeni watazitimiza ambapo ameahidi kushirikiana na waliokuwa wagombea wengine wa nafasi mbalimbali lakini bahati mbaya kura hazikutosha
"La kwanza lilikuwa kuleta mshikamano na kuirudisha timu kwa Wananchi"
"La pili lilikuwa kubadilisha mfumo na uendeshaji wa timu. Nawaahidi mbele yenu hili tutalifanya ndani ya mwaka mmoja au chini ya hapo"
"La tatu muhimu tutasaidia miradi inayoendelea klabuni sasa ambayo ni ujenzi wa uwanja, ukarabati wa jengo na miradi mipya"
"Nafurahi Igangula hapa amesema yuko tayari kutoa ushirikiano, niliona randama yake wakati wa kampeni, nawaahidi tutashirikiana nae na tutahakikisha atakuwa sehemu ya uongozi wetu"
"Dk Tiboroha ameshindwa kufika hapa kutokana na kuchelewa kutoka safarini Arusha lakini ameahidi kuchangia Tsh Milioni Moja kwa ajili ya shughuli mbalimbali za klabu, na yeye tuko nae pamoja"
"Muhimu nimeomba sote tuvunje makundi yetu baada ya uchaguzi. Umoja na Ushirikiano wetu utatusaidia kusonga mbele kwa haraka"cut
UTAWALA BORA
Dk Msolla amesema katika uongozi wake watahakikisha wanafuata utawala bora na watakuwa makini katika usimamizi wa fedha
"Maeneo ya ukaguzi wa ndani na nje tutakuwa wakali sana. Tutakuwa tayari kutumia gharama kuwapata wakaguzi wanaoheshimika Kimataifa na tutakuwa tukitoa ripoti wazi kwenye vyombo vya habari kuhusu mapato na matumizi ya klabu kama zinavyofanya taasisi nyingine"
KUIMARISHA KIKOSI CHA YANGA
Dk Msolla amesema kwa ushirikiano ulioonyeshwa na makundi mbalimbali ya Yanga, ndani ya wiki mbili au tatu, zoezi la kukiboresha kikosi litakuwa limeanza
"Nawaahidi ndani ya wiki mbili au tatu zijazo, tutaanza kutengeneza kikosi imara chini ya usimamizi wa kocha Mwinyi Zahera"
0 Comments