Windows

Zahera Kumtangaza Mkude Yanga Jumanne

Jonas Mkude,

KAMA Yanga kweli wapo siriazi, mashabiki wa Simba wanaweza kukumbwa na mshtuko mkubwa Jumanne ijayo pale Mwinyi Zahera atakapoweka mambo yake hadharani.

 

Habari za ndani ambazo Championi Ijumaa limezipata jana ni kwamba vigogo wa Yanga wamepania kumng’oa Mkude ndani ya Simba tena kwa dau kubwa.

 

Habari zinasema kwamba Yanga wamemwambia Mkude na mwanasheria wake kwamba wako tayari kutoa Sh mil 120 kijana atue Jangwani na wamemhakikishia kwamba mambo yanakwenda kuwa mazuri Yanga wala asihofu.

Mwinyi Zahera

Habari zinasema kwamba Yanga wamepania kumchukua mchezaji huyo ambaye mkataba wake na Simba unamalizika Jumanne na bado hajasaini mpya.

 

Ingawa Simba jana Alhamisi ilikuwa kwenye harakati za kumalizana na wachezaji wao wote ambao kocha amesisitiza wabaki, ishu ya Mkude ilikuwa ngumu kwani bado anasikilizia upepo na wao wamekuwa hawana haraka naye kwa vile wanaamini atabaki kwa ushawishi wa Mo.

 

“Safari hii uongozi umeamua kuhakikisha unamsajili Mkude kwani kila kitu kipo sawa na kilichobakia tu ni yeye kusaini,” kilisema chanzo cha uhakika ndani ya uongozi.

“Kwa fedha aliyotengewa ni vigumu kuiachia labda Simba wampatie zaidi ya hiyo jambo ambalo naamini hawawezi kulifanya. “Uongozi wetu upo tayari kutoa Sh 120 milioni kwa ajili ya kumsajili lakini pia kwa
mwezi atakuwa akilipwa mshahara mzuri tofauti na ule anaochukua Simba kwa sasa,” kilisema chanzo chetu.

 

Alipoulizwa Mkude mwenyewe kuhusiana na ishu hiyo alisema: “Kwa sasa sipo tayari kusema chochete juu ya suala hilo ila mkataba wa Simba ni kweli unamalizika hivi karibuni na bado sijasaini mkataba mwingine. “Mengine yatafuata ila bado sijasaini mkataba kama ambavyo imekuwa ikisemwa.

 

” Hata hivyo, Mwanasheria wa Mkude, ambaye hakutaka kutajwa jina lake gazetini alipoulizwa kuhusiana na ishu hiyo alisema: “Ni kweli Yanga wanamtaka na wametoa ofa yao nzuri tu lakini bado hatujaamua ni wapi ataenda kwa sababu ana ofa nyingine kutoka Morocco pamoja na Misri.

 

“Hata hivyo, majibu zaidi juu ya ishu hiyo nitafute Jumapili nitakuwa na kitu cha uhakika cha kukwambia.” Championi linajua kwamba leo na kesho Mkude atakuwa na mazungumzo ya kina na pande zote mbili.

 

Kwa upande wake Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, Omary Kaya alisema: “Hilo siwezi kulizungumzia kwa sababu mambo yote yanayohusiana na usajili kocha ndiye anayejua, kwa hiyo muulize kocha.”

 

Alipotafutwa Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera alisema: “Ukweli wa hilo utajulikana Mei 28, mwaka huu ambapo nitakuwa tayari nimekamilisha zoezi zima la usajili.

 

“Natarajia kusajili wachezaji nane, wawili kati ya hao ni wa kutoka hapa nchini, kwa hiyo tusubiri tuone kama na yeye atakuwa ni mmoja kati ya wachezaji hao.”

The post Zahera Kumtangaza Mkude Yanga Jumanne appeared first on Global Publishers.


Post a Comment

0 Comments