Windows

Zahera avuta wawili Yanga, Kabunda ndani

Mwanaspoti, Michezo, Michezo blog, Zahera, avuta, wawili, Yanga, Kabunda ndani, MICHEZO, Mwanasport
 Kikosi cha Yanga leo Jumatatu kinatarajiwa kushuka kwenye Uwanja wa Samora, mjini Iringa ikiwa na nguvu mpya, si mnajua jana klabu hiyo ilifanya Uchaguzi Mkuu wa kupata viongozi wapya, huku nyuma Kocha wake Mwinyi Zahera ameanza mambo mapema.


Zahera tayari amenasa majina ya wachezaji anaowataka kwa ajili ya msimu ujao, ambapo licha ya kuwa na orodha ya nyota wa kigeni, lakini faili lake lina majina ya mawinga wawili matata wanaocheza hapa nchini.


Ingawa Zahera amekuwa msiri wa majina ya wachezaji alionao, lakini nusanusa za Mwanaspoti zimebaini moja ya jina ni la winga machachari wa KMC, Hassan Kabunda ambaye Jangwani walikuwa wakimvizia toka msimu uliopita alipokuwa Mwadui.


Akizungumza na Mwanaspoti kabla ya Yanga kwenda Iringa, Zahera alisema usajili anaotaka kuufanya kwa sasa ni wa kutatua mapungufu yalipo kwenye kikosi cha sasa na kwamba mpango wake ni kuwavuta mawinga wawili wenye mbio na uwezo mkubwa kisoka.


Kwa sasa Yanga imekuwa ikiwategemea Mrisho Ngassa na Deus Kaseke kucheza kama mawinga wa timu hiyo, lakini hawaanzi pamoja, huku Pius Buswita akikosa nafasi kikosi cha kwanza na tatizo kubwa lipo winga ya kushoto.


"Mawinga hao wawili mbali ya kuwa na sifa za kukimbia na kumiliki mpira, lakini nataka wawe na uwezo wa kufunga wenyewe muda mwingine na nikiwapata, Yanga msimu ujao eneo la mbele hasa pembeni litakuwa tishio na kuzalisha mabao mengi," alisema.


"Ukiangalia mechi nyingi msimu huu kuna ambazo zilionekana kuwa ngumu lakini kuna nafasi nyingi ambazo tulitengeneza kupitia pembeni, lakini mawinga wangu walishindwa kufika katika eneo husika la kushambulia kwa wakati na tukashindwa kupata mabao ya kutosha, hilo nimeliona na ndio maana litakuwa sehemu ya kulifanyia kazi kwenye usajili.


"Kama mambo yanatakwenda sawa kama tulivyopanga na uongozi kabla ya msimu ujao kuanza tutakuwa tumeswhamaliza kufanya usajili wa maeneo yote ambayo tutakuwa tunataka kuongeza nguvu kwani kuna baadhi ya wachezaji nimeshaongea nao ili kupunguza presha ya kufanya usajili kipindi cha mwisho," alisema Zahera.


Zahera amekuwa na jeuri ya usajili mpya kwa msimu ujao baada ya kuanzishwa harambee ya kusaka Sh 1.5 bilioni kupitia Kamati ya Hamasa na Michango iliyo chini ya Mbunge na Waziri, Anthony Mavunde.


Katika dirisha dogo Yanga ilikuwa ikiwanyemelea saini za mawinga Charles Ilanfya aliyekuwa Mwadui kabla ya kutua KMC, pia ilimleta Ruben Bomba kutoka DR Congo kabla ya kushindwa kumsainisha kwa sababu ya kifedha.


Yanga pia imehusishwa kuwapigia hesabu mabeki wa Simba, Nicholas Gyan na Juuko Murshid ambao mikataba yao inamalizika, huku pia ikitajwa kumleta kipa Farouk Shikalo wa Bandari Kenya na straika Mzimbabwe, Roderick Mutuma aliyepo FC Lupopo wa DRC.


Post a Comment

0 Comments